
Dodoma. Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) lipo kwenye hatua za manunuzi za mradi wa kuagiza na kusimika vituo vya Gesi Asilia (CNG) vinavyohamishika katika barabara ya Dar es Salaam kuelekea Dodoma.
Hatua hiyo ni kuboresha upatikanaji wa gesi hiyo kwa mikoa iliyo katika barabara kuu kuelekea Dodoma.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dustan Kitandula amesema hayo leo Jumatano Februari 12, 2025 wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Grace Tendega kwa niaba ya Waziri wa Nishati.
Tendega ametaka kufahamu ni Serikali ina mkakati wa kuhakikisha magari ya Serikali yanakuwa na mfumo wa nishati ya gesi.
Akijibu swali hilo, Kitandula amesema ili kuwezesha Serikali kuanza kutumia magari yanayotumia gesi, Serikali imejikita kuweka miundombinu ya kuwezesha matumizi ya CNG kwenye magari ya serikali kwa urahisi.
Amesema Serikali kupitia Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA) imeshaanza taratibu za kuweka miundombinu kwa ajili ya magari ya Serikali yatakayotumia gesi ikiwemo kufanya tathimini za athari za kijamii na mazingira pamoja na uandaji wa michoro ya kina ya kihandisi na usimamizi wa ujenzi.
Amesema taratibu hizi ni kuweka miundombinu rafiki kwa magari ya serikali kuanza kutumia gesi kwenye magari (CNG).
Aidha, Kitandula amesema ili kuboresha upatikanaji wa CNG kwa mikoa iliyo katika barabara kuu kuelekea Dodoma, TPDC ipo kwenye hatua za manunuzi za mradi wa kuagiza na kusimika vituo vya CNG vinavyohamishika ambapo kwa kuanzia vitatu vitasimikwa Dar es Salaam kimoja kitasimikwa Morogoro na viwili vitasimikwa Dodoma.
Katika swali la nyongeza mbunge huyo amehoji Serikali haioni haja ya kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha magari yanayotumia gesi yanaweza kuingizwa moja kwa moja nchini.
“Kufunga mfumo wa gesi katika magari ni gharama kubwa sana ni takribani Sh2 milioni hadi Sh3 milioni, Watanzania walio wengi wanashindwa kumudu, je, Serikali haioni haja ya kupunguza kodi kwenye vipuri ambavyo vinatumika kufunga gesi katika magari kwa sababu hakuna hata kiwanda cha kipuri hapa Tanzania,” amehoji.
Akijibu swali hilo, Kitandula amesema katika kuhamasisha magari yanayotumia gesi asilia na katika kuhakikisha wanaweka mazingira rafiki kwa sekta binafsi kushiriki, Bunge litakumbuka mwaka 2023/24 Serikali ilifuta kodi ya ushuru wa bidhaa kwa magari yote yanayoingizwa nchini yakiwa na mfumo unaotumia gesi asilia.
“Katika hili tayari taasisi mbalimbali zikiwemo za Serikali na sekta binafsi zimeanza kunufaika Januari taasisi yetu ya mabasi yaendayo kwa kasi imeidhinishiwa magari 755 yaagizwe yaweze kuingia nchini yakiwa na mfumo wa gesi asilia. Na tayari zabuni hiyo imeshatangazwa,”amesema.
Kuhusu kupunguza bei katika vipuri, Kitandula amesema kwa sasa Serikali kupitia Wizara ya Fedha, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na TPDC na Wizara ya Nishati wapo katika mapitio ya maeneo ambayo wanaweza kupata msamaha wa vipuri vya kuunganisha mfumo wa gesi asilia ili viweze kupatikana kwa bei rahisi.
Amesema pia TPDC ipo katika mkakati wa kutafuta wawekezaji wa vipuri hivyo watakaoweza kuweza viwanda nchini ili viweze kupatikana kwa urahisi.