Tovuti ya Russia: Biden anaweza kuanzisha vita vya dunia iwapo Harris atashindwa katika uchaguzi

Kituo cha Kimkakati cha Russia cha Tamaduni kimetazamia kuwa Rais wa Marekani Joe Biden yumkini atazua mzozo wa kimataifa katika kipindi cha miezi miwili iliyosalia ya utawala wake, iwapo naibu wake, Kamala Harris, atashindwa katika uchaguzi wa rais.

Kituo hicho kimesema – katika ripoti yake – kwamba viashiria vya kwamba Washington ina nia ya kuzidisha mzozo wa kimataifa vinadhahiri katika kuimarishwa uwepo wa majeshi ya Marekani katika Mashariki ya Kati na Ulaya.

Mwandishi wa kituo hicho amesema kwamba, Pentagon imetangaza nia yake ya kutuma Mashariki ya Kati mifumo zaidi ya ulinzi wa makombora, kikosi cha ndege za kivita, ndege za kujaza mafuta na ndege kubwa za kivita za masafa marefu za Jeshi la Anga, aina ya B-52 Stratofortress, sambamba na kupeleka mfumo wa ulinzi wa kukabiliana na makombora wa THAAD kwa ajili ya kuilinda Israel.

Kituo cha Kimkakati cha Russia cha Tamaduni kimesema kuwa uongozi wa jeshi la Marekani huko Ulaya umetangaza kwamba, Pentagon itapeleka ndege za kivita za kimkakati huko Ulaya kufanya operesheni ya pamoja na mafunzo ya kutumia ndege za kivita za Marekani na washirika wa NATO.

Itakumbukwa kuwa, baada ya mkutano wa kilele uliofanyika Vilnius mwezi Juni 2023, wanachama wa NATO walikubali kutoa mafunzo kwa wanajeshi 300,000 na kuwaweka katika hali ya tahadhari kwa ajili ya kuulinda muungano huo dhidi ya eti hatari ya Russia.