Tofautisha, ukorofi na utundu wa mtoto wako

Huenda wewe ni miongoni mwa wazazi waliochoshwa na ukorofi wa watoto wao.

Ukorofi ni ile hali ya kutokutambua mamlaka, kutokusikia maelekezo halali, tabia inayoweza kutafsirika kama uasi wa mara kwa mara dhidi ya mamlaka ya mzazi.

Tunazungumzia watoto wenye ujasiri kupita mipaka, watoto wanaoweza kukukatalia jambo na wala wasijisikie wamekukosea. Ikiwa una mtoto unayeweza kumuonya na asisikie, huyo ndiye tunayemwita mtoto mkorofi.

Ukorofi ni kushindana

Ukorofi, kwa kawaida, huenda sambamba na tabia ya kupenda kujiona ni mtawala anapokuwa na wenzake.

Anaweza kuwa mwongeaji au mkimya lakini anafurahia kuona wenzake wakifanya kile anachokitaka yeye.

Ni aina fulani ya hulka ya uongozi iliyochanyikana na kutokuelewa wengine wanataka nini.

Mtoto wa hivi huwa mgomvi anapokuwa na wenzake. Tabia yake ya kushindana na watu humfanya ajikute kwenye migogoro ya mara kwa mara.

Ukiwa na mtoto wa namna hii kupokea mashtaka ya mara kwa mara kwamba kapigana na mwenzake linakuwa jambo la kawaida.

Shuleni mtoto wa hivi huwa hafanyi kazi anazopewa, hatulii darasani na muda mwingi anautumia kusababisha mitafuku na wenzake, hat ana walimu, tena pasi na sababu za msingi.

Matokeo ya haya yote, ni kuzorota kwa maendeleo yake kitaaluma shuleni.

Ukorofi wa mtoto huanza kuonekana tangu akiwa na umri mdogo.

Mtoto mkorofi hutumia lugha ya kurusha rusha mikono na miguu kama namna ya kupinga unachowaelekeza kufanya. Hulia lia bila sababu zinazoeleweka na ni vigumu kumnyamazisha.

Ukimwambia asichokitaka anaweza kususa, akaamua kukunyamazia kama namna ya kukushinikiza ubadili msimamo wako.

Kwa hakika huyu ni mtoto anayeweza kukuaibisha hata mbele za watu.

Mnaweza Kwenda dukani, akaamua kulilia kitu ambacho hamkukubaliana kukinunua na usipokaa sawa utaishia kukinunua kwa ajili yake.

Tena wakati mwingine atavizia ukiwa na watu unaowaheshimu, wageni wako mathalani, na atakushikia bango kwa jambo lake na hutokuwa na namna ya kumkatalia. Ikiwa kuna nyakati nyingi unajikuta ukibadili msimamo kwa ajili ya kukidhi matakwa ya mtoto, huenda unashughulika na mtoto mkorofi.

Utundu ni udadisi

Ukorofi ni tabia tofauti kidogo na utundu. Utundu ni tabia inayoenda sambamba na uchangamfu wa akili anaokuwa nao mtoto. Mtoto mtundu anafikiri.

Unapomwambia jambo atalihoji kuonesha anatafakari kile unachomwambia.

Mtoto mdadisi atakuuliza maswali mengi yanayolenga kutaka kuelewa. Udadisi wake unamfanya awe na kiu ya kufahamu mambo yanayomzunguka, hali inayoweza kutafsirika kama ubishi.

Unapokuwa na mtoto mtundu, kuna wakati utahisi anajaribu kupingana na maagizo yako kama mzazi.

Mtoto anapofikiri kile anachoambiwa hakiendani na kile anachotamani kuna namna fulani atakuwa na kaubishi ambacho ni tofauti na ukorofi tunaouzungumzia hapa.

Mtoto mwenye akili njema mara nyingi hapokei kirahisi kile anachoambiwa bila kukitafakari. Utamwambia fanya hiki na anaweza kukuweka kwenye mazingira ya kuonesha sababu kwa kuuliza maswali. Kuchukulia maswali mengi unayoulizwa na mwanao kama ukorofi inaweza isiwe sahihi sana.

Udadisi, kwa kawaida, unadai mantiki ambayo si wazazi wengi huweza kuvumilia.

Udadisi unadai kuchagua kati ya machaguo kadhaa yaliyopo hali inayoweza kutafsiriwa kama kubishana na mzazi.

Tatizo la utundu ni pale inapofikia mahali mtoto hatambui mamlaka ya mzazi.

Kutokutambua mamlaka ya mzazi kunaleta tatizo la kufikiri anaweza kuwa na msimamo mkali kwa kile anachokiamini kiasi kwamba hawezi tena kuambiwa jambo akaelewa, hawezi kufikiri mwenzake anajisikiaje, anakuwa mbabe na mwenye hulka ya kujiona mtu bora kuliko watu wengine wote.

Ukubwani, ukorofi wa kiwango hiki unahatarisha uhusiano baina ya watu.

Unapokuwa mtu mkorofi, huwezi kujisikia hatia kumwumiza mwezako. Tena wakati mwingine furaha yako inaweza kuwa kuona wenzako wanaumia.