TMDA yateketeza dawa za mamilioni ya fedha, yaonya wafanyabiashara

Geita. Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Ziwa Magharibi, imeteketeza dawa zenye thamani ya Sh34 milioni sawa na kilo 1,000 zilizobainika kwisha muda wake, kuingizwa nchini kinyemela na zile ambazo hazijasajiliwa.

Akizungumza leo Jumapili Machi 30, 2025 wakati wa uteketezaji wa dawa hizo, Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa Magharibi, Dk Edger Mahundi amesema dawa hizo ni hatari kwa afya ya watumiaji.

Amesema dawa zisizosajiliwa zinahatarisha afya ya watumiaji kwa sababu ubora na usalama wake haujulikani na zile zilizokwisha muda wa matumizi hubadilika na kuwa sumu mwilini na zingine husababisha saratani.

Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa Mangharibi, Dk Edger Mahundi akizungumza wakati wa uteketezwaji wa dawa zilizokamatwa.

“Dawa zilizokwisha muda wake au zisizosajiliwa zinaweza kusababisha madhara makubwa kiafya, hata kupelekea kifo, huwa tunasikia malalamiko ya watu kudhurika na dawa hii ni moja ya sababu,” amesema na kuongeza;

“Dawa isiyosajiliwa inaweza kuwa bandia au yenye viambato visivyo sahihi, hivyo badala ya kutibu inazidi kumdhoofisha mgonjwa.

Kwa mujibu wa DK Mahundi, zipo dawa zilizokamatwa kwenye mipaka ya Rusumo, Kyerwa na Mtukula ambazo zilibainika baada ya ukaguzi kuwa hazina sifa.

“Tumekamata pia dawa zinazouzwa kwenye majengo yasiyo na sifa lakini pia zinauzwa na watoa dawa wasio na sifa, pia tumeziondoa maana tukiziacha wataendelea kuziuza na ni hatari kwa afya na usalama wa mgonjwa,” amesema Dk Mahundi.

Akizungumzia hatua zilizochukuliwa Dk Mahundi amesema katika operesheni hiyo, mtu mmoja alikamatwa akihusishwa na kughushi tarehe za mwisho za matumizi ya dawa na tayari amefikishwa mahakamani na kesi inaendelea.

TMDA imewataka wananchi kuhakikisha wananunua dawa katika maduka yaliyoidhinishwa na kuhimiza wafanyabiashara kuzingatia taratibu ikiwemo kutumia watoa dawa wenye sifa.

Mamlaka hiyo imesisitiza kuwa itaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha dawa zinazoingizwa na kuuzwa nchini ni salama kwa matumizi.

Mmoja wa wamiliki wa maduka ya dawa, Masumbuko Kameza amesema tamaa ya kupata kipato ndio sababu za baadhi ya wafanyabiashara kuuza dawa zilizoisha muda wake.

Amesema biashara ya dawa za binadamu inahusisha uhai wa mtu na kuwataka wafanyabiashara wenzake kutii sheria na taratibu zilizowekwa ili kuepusha mgonjwa na kupata madhara yanayoweza kusababisha kifo.

Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Octavianus Robert amesema matumizi ya dawa zilizokwisha muda au zisizosajiliwa ni hatari kwa matumizi ya binadamu kwani badala ya kuponya zinaweza kusababisha kifo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *