TMA yatangaza uwepo wa kimbunga Jude

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeeleza uwepo wa kimbunga Jude katika Bahari ya Hindi, eneo la Rasi ya Msumbiji.

TMA kupitia taarifa yake iliyoitoa leo Jumatatu Machi 10, 2025, ikieleza kupitia uchambuzi wa mifumo ya hali ya hewa unaonyesha kuwa kimbunga hicho kitaingia nchi kavu katika eneo la Msumbiji mchana wa leo na kupungua nguvu yake.

“Kimbunga Jude kinatarajiwa kurejea tena baharini na kuimarisha nguvu yake katika kipindi cha kati ya Januari 13 hadi Machi 15, 2025. Kutokana na mwelekeo na umbali wake, Kimbunga Jude hakitarajiwi kuwa na athari za moja kwa moja hapa nchini,” imeeleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa TMA, uwepo wa kimbunga hicho eneo la Rasi ya Msumbiji unatarajiwa kuchagiza mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na kusababisha ongezeko la mvua katika maeneo mbalimbali.

Taarifa hiyo ya TMA inaeleza kuwa uwepo wa kimbunga hicho unaambatana na kuanza kwa msimu wa mvua za masika 2025 katika maeneo yapatayo misimu miwili ya mvua kwa mwaka.

“Tunashauri watumiaji wa bahari na jamii kwa ujumla kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka TMA na kupata ushauri na miongozo ya wataalamu wa kisekta.

“TMA inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga Jude na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi,” imeandikwa kwenye taarifa hiyo.

Ikumbukwe Januari 2025, TMA ilionya pia uwepo wa kimbunga Dikeledi katika bahari ya Hindi mwambao wa Pwani ya Msumbiji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *