
Mbeya. Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini imewataka wavuvi wa Ziwa Nyasa Wilaya ya Kyela mkoani hapa kuchukua tahadhari kufuatia kuwepo kwa mvua ya mawe itakayoambatana na upepo mkali, mawimbi na wingu la radi.
Pia, wavuvi hao wametakiwa kuepuka kasumba ya kutumia njia za jadi kutabiri athari za majini kwa ajili ya kuendelea na shughuli za uvuvi.
Meneja wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) Kanda, Elias Lipiki ameliambia Mwananchi Digital leo Jumatano Februari 12, 2025 alipohojiwa kuhusiana na utabiri wa athari za shughuli za uvuvi katika Ziwa Nyasa.
“Awali mvua zilichelewa kunyesha zilianza mwishoni mwa mwezi Desemba, 2024 na zinatarajiwa kuisha mwanzoni kwa mwezi Mei, 2025 katika maeneo ya maziwa kutakuwa na dhoruba itakayo sababisha wingu kubwa la radi, upepo mkali na mawimbi yenye uwezo mkubwa wa kupindua vyombo vya majini na kusababisha madhara kwa wavuvi,” amesema.
Lipiki amesema ili kukabiliana na hali hiyo umefika wakati wavuvi kutopuuza utabiri wa hali ya hewa, licha ya kuwa na mifumo yao binafsi ya kutumia ujuzi wa njia za jadi ambazo sio salama kwao.
“Kipindi hiki ni hatari sana kwa wavuvi kuingia majini kufuatia kuwepo na upepo mkali unao ambatana na mawimbi makubwa, wingu la radi hali ambayo inaweza kuleta athari ya kuzama mitumbwi, vifo, majeruhi na nyumba kuezuliwa,” amesema.
Amesema vipindi vya dhoruba majini utokea kuanzia majira ya alfajiri kunapoanza kukucha mpaka saa tisa alasiri na kudumu kwa muda wa nusu saa majini.
Ametaja sababu ya kutokea hali hiyo ni kutokana na uwepo wa wingu la radi katika maeneo ya maziwa hususani kwa Ziwa Nyasa Mkoa wa Mbeya.
Kuhusu athari kwenye uzalishaji, Elias amesema wakulima watumie fursa ya uwepo wa mvua hizi kuendelea kuzalisha kutokana na udongo kuwa na wingi wa maji ya kutosha.
“Changamoto ipo kwa upande wa utekelezaji wa miradi hususani ya ujenzi wa barabara na vinginevyo wakandarasi wachukue tahadhari kubwa katika kipindi hiki ambacho siyo rafiki kuweza kukamilisha kufuatia uwepo wa mvua nyingi zinazo tarajiwa kuisha mwanzoni mwa mwezi Mei mwaka huu,” amesema.
Wakati huo huo amesema utabiri umeonyesha kipindi cha wiki mbili sasa mito imeanza kujaa maji na kuhatarisha wananchi wanaoishi mabondeni.
“Maeneo mengi ya mito imeonyesha ongezeko la maji na kuna uwezekano wa kina kuongezeka kufuatia mvua zinazo endelea kunyesha ni vyema wananchi wa maeneo ya mabondeni kuchukua tahadhari,” amesema.
Amesema kufuatia hali hiyo, TMA wako kwenye mikakati ya kutumia mfumo wa utoaji taarifa za hali ya hewa kupitia mitandao ya simu za mkononi kwa wavuvi na wananchi ili wachukue tahadhari mapema.