TLS yashauri mali za Serikali zikatamatwe, Mahakama yajibu

Mbeya. Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimeshauri mambo kadhaa ya kufanyia kazi kufanikisha mpango wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ikiwa ni pamoja na kuondoa zuio la kukamata mali za Serikali ili kuhakikisha haki inatendeka.

Akizungumza leo Jumatatu, Februari 3, 2025, wakati wa kilele cha Wiki ya Sheria mkoani Mbeya, Mwenyekiti wa TLS Nyanda za Juu Kusini, Baraka Mbwilo, amesema ili kufikia malengo ya dira hiyo, lazima changamoto zilizopo zifanyiwe kazi.

Amesema kumekuwepo na ucheleweshaji wa mashauri mahakamani, na wananchi wengi hupeleka malalamiko yao katika vyombo visivyo sahihi, hususan kwa wanasiasa, hali inayochelewesha haki.

Pia ametaja gharama za kufungua kesi na utaratibu wa kusamehewa kuwa mgumu hasa kwa wasio na kipato, huku akiongeza kuwa uchache wa mabaraza ya ardhi kunasababisha malalamiko mengi.

“Kuna muda mahakama inaweka mazuio yasiyo ya msingi, hasa kwenye mashauri ya benki, ambapo mtu akikopa na kushindwa kulipa, anapewa notisi na taarifa zote zinazostahili, lakini anaishia kutekeleza.

“Tatizo kubwa ni ukazaji wa hukumu za Serikali. Mtu anaomba tenda ya kusambaza vifaa serikalini na haijalipwa, anakwenda mahakamani kuomba haki ya kulipwa, lakini kwenda kukazia hukumu haruhusiwi kukamata mali za Serikali,” amesema Mbwilo na kuongeza kuwa sheria kama hizo hazifai.

Amesema kuwa ikikamatwa mali za Serikali, itapelekea uwajibikaji na wazembe wataondoka, huku akisisitiza kuwa nchi haiwezi kuendelea kama kutakuwa na kikwazo cha kisheria katika kutekeleza majukumu ya Serikali.

Mbwilo pia ameongezea kuwa kumekuwepo na utitiri wa vyombo vingi vya mashauri, jambo linalodhoofisha ufanisi, kwani baadhi yao vina urasimu na ukosefu wa wataalamu.

Ametoa wito wa kuongezwa kwa elimu ya sheria kwa wananchi na kuhimiza ushirikiano na kampeni ya Mama Samia Legal Aid.

“Kuna vyombo ambavyo haviheshimu taaluma ya sheria, na hiki ni chombo pekee duniani kilicho na mamlaka ya kuamua. Lazima tuheshimiwe na hakimu atakapotoa amri kwa mujibu wa sheria, kama hujaafiki, kata rufaa na tupeni uhuru,” amesema Mbwilo.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya, Joachim Tiganga, amesema kuwa katika Wiki ya Sheria wamefikia na kuzidi malengo waliyojiwekea kwa kutoa elimu kwa wananchi 5,756.

Amesema Mahakama imejipanga kuboresha miundombinu yake ili kuhakikisha watu wote wanapata haki zao, kwani ni chombo kilichopewa jukumu hilo.

“Niwaombe wananchi kutumia fursa ya mahakama inayotembea kupata huduma badala ya kuwa na hofu kwamba inagharimu, kwani huduma hiyo ni sawa na kuwa ofisini,” amesema.

Ameeleza pia kuwa mazuio yanayotolewa na Mahakama mara nyingi huombwa na mawakili wa kujitegemea, hivyo kama Mbwilo ameona kuna tatizo, ataenda kupeleka ujumbe kwa wenzake ili Mahakama iendelee kusikiliza mashauri.

Mmoja wa wananchi walioshiriki maadhimisho hayo,  Maua Juma, amesema pamoja na Mahakama kuboresha huduma zake, bado wapo wananchi hawafikiwi ipasavyo.

“Mfano, teknolojia ya mahakama inayotembea inaishia zaidi maeneo ya mjini, lakini wahudumu hawafiki kwenye vijijini, Serikali inagharamia mafuta lakini huduma inabaki mjini,” amehoji.

Naye Charles Mbela amesema kuwa Wiki ya Sheria inapaswa kuadhimishwa maeneo ya vijijini, sehemu za wazi badala ya kufanyika mjini kwenye ofisi za Mahakama.

“Kuna watu wanaogopa kwenda kwenye ofisi kama Mahakama au Polisi, hivyo hizi sherehe ziwe zinafanyika maeneo ya wazi ili wananchi wengi washiriki, na hii itasaidia kuweka ukaribu kati ya mamlaka na wananchi,” amesema Mbela.