Tishio la Houthi Yemen: Marekani yalazimika kukwepesha shughuli zake katika Bahari Nyekundu

Robo tatu ya wasafiri wa baharini wa Marekani wanaopitia Bahari Nyekundu sasa wanalazimika kuzunguka eneo hilo na kupitia kusini mwa Afrika kutokana na mashambulizi ya Wahouthi nchini Yemen, mshauri wa Ikulu ya White House amesema siku ya Jumapili, Machi 23.

Imechapishwa: Imehaririwa:

Dakika 3

Matangazo ya kibiashara

“Asilimia 75 ya meli zetu zenye bendera ya Marekani lazima zipitie pwani ya kusini mwa Afrika badala ya Mfereji wa Suez,” Mike Waltz, mshauri wa usalama wa taifa wa Donald Trump, amesema kwenye CBS.

Katika mazungumzo ya simu na Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio pia “ameelezea azma ya serikali ya [Marekani] kurejesha uhuru wa usafiri wa baharini katika Bahari Nyekundu kupitia operesheni za kijeshi dhidi ya Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran,” ofisi yake imesema katika taarifa siku ya Jumapili.

Siku ya Jumatano Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema kwamba “katika kipindi cha miezi 18 iliyopita, Wahouthi wamepiga au kushambulia Jeshi la Wanamaji la Marekani mara 174, na kushambulia meli za kibiashara mara 145. “

Wahouthi wanasema wanafanya kazi kwa mshikamano na Wapalestina huko Gaza

Yemen ambayo ni nchi maskini kwenye rasi ya Uarabuni, imekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 2014 ambavyo vimesababisha vifo vya mamia kwa maelfu ya watu na kusababisha maafa ya kibinadamu. Tangu kuanza kwa vita katika Ukanda wa Gaza, vilivyochochewa na shambulio la Hamas dhidi ya Israeli mnamo Oktoba 7, 2023, Wahouthi, ambao wanadhibiti maeneo makubwa ya Yemen, wamefanya mashambulio kadhaa ya makombora dhidi ya Israeli na meli zinazotuhumiwa kuwa na uhusiano na Israeli, wakidai kufanya kazi kwa mshikamano na Wapalestina.

Kufuatia kuanza kutekelezwa kwa makubaliano dhaifu ya usitishwaji mapigano huko Gaza mnamo Januari 19, Wahouthi, wakiungwa mkono na Iran, walikuwa wamesitisha mashambulizi yao. Lakini mnamo Machi 11, walitangaza nia yao ya kuanzisha tena mashambulizi yao katika pwani ya Yemen, baada ya Israeli kukataa kuruhusu msaada wa kibinadamu kuingia katika ardhi ya Palestina.

Katika hali hiyo, Marekani imekuwa ikifanya mashambulizi katika ngome za waasi kwa zaidi ya wiki moja, ikiwa ni mara ya kwanza tangu Donald Trump aingie madarakani Januari 20. Siku ya Jumapili waasi wa Houthi wa Yemen pia walidai kwamba mtu mmoja aliuawa na wengine kumi na watatu kujeruhiwa katika shambulio katika mji mkuu wa Sanaa ambapo walidai kuwa ulifanywa na Marekani, kulingana na taarifa iliyotolewa Jumapili jioni na Wizara yao ya Afya.

Marekani haijathibitisha kufanya shambulio hilo, lakini afisa wa Pentagon ameliambia shirika la habari la AFP kwamba “Centcom inaendesha mashambulizi, usiku na mchana, dhidi ya maeneo mengi ya Houthi inayoungwa mkono na Iran nchini Yemen.” Kamandi Kuu ya Marekani imerisha video kwenye ukurasa wake wa X za ndege za kijeshi zikipaa kwenda “kurejesha Uhuru wa Urambazaji.”

“Rais Trump ameamua kuwapiga Houthis na kuwapiga vikali, tofauti na utawala uliopita” wa Joe Biden, Mike Waltz amedai kwenye kituo cha  CBS siku ya Jumapili. “Funguweni na muache wazi njia za baharini, endelesheni biashara, ni kipengele cha msingi cha usalama wa taifa letu,” mshauri huyo wa Ikulu ya White House amesema, akijibu Wahouthi ambao “wana makombora ya hali ya juu, makombora ya balestiki, na baadhi ya ulinzi wa hali ya juu zaidi wa anga, zote zinazotolewa na Iran.” 

Wiki moja kabla, alidai kwamba mashambulizi ya Marekani kwenye ngome za Wahouthi yamewaangamiza wanachama kadhaa wakuu wa vuguvugu hilo. Wahouthi, kwa upande wao, waliripoti kuwa watu 53 waliuawa na 98 kujeruhiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *