Geita. Watu watano akiwemo mtoto mwenye umri wa wiki mbili wamenusurika kufa baada ya mtambo aina ya tingatinga (bulldozer) kuparamia nyumba tatu za wananchi katika kitongoji cha Isangiro kata ya Rwamgasa wilayani Geitaza usiku wa kuamkia leo Aprili 3, 2025 wakiwa wamelala.
Mtambo huo unaomilikiwa na kampuni ya chimbaji madini ya dhahabu ya Bucreef unaelezwa kuparamia nyumba tatu za watu baada ya dereva aliyekua akiuendesha kuruka na kukimbia na kuucha ujiendeshe wenyewe umbali wa zaidi ya kilomita moja.
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba akizungumza na wananchi wa Isangiro baada ya kufika eneo hilo amesema dereva aliyekuwa akiuendesha alibainika kuiba mafuta na alipojua anafuatiliwa aliamua kuuacha kisha kukimbia.
“Uchunguzi wa awali unaonyesha mwendeshaji wa mtambo huo (Operator) alijihususha na wizi wa mafuta na alikua na watu wawili baada ya watu wa mgodi kujua kuna wizi alianza kuondoka na alipogundua nafuatiliwa aliruka na kuacha ukajiongoza wenyewe ,”amesema Komba.
Komba amesema usiku wa saa nane mtambo huo uliparamia nyumba za wananchi wakiwa wamelala na kuvunja kuta. “Hata kupona kwa wananchi hawa ni muujiza wa Mungu.
“Huu mtambo umetembea zaidi ya kilomita moja ukiwa hauna mwongozaji umegonga nguzo kadhaa za umeme, umepita kwenye nyumba za watu hakika waliopona ni bahati mashuhuda mmefika hapa na kukuta unanguruma maana umetengenezwa kwa mfumo ambao unaweza kujiendesha wenyewe hata kuuzima imebidi mtaalamu anyofoe kifaa ili uzime.

Baadhi ya nyumba iliyo haribiwa na bulldozer katika kitongoji cha Isangiro Kata ya Rwamgasa Wilaya ya Geita.
“Alichofanya huyu opereta ni zaidi ya unyama, aliruka kwenye gari na kuacha gari likijiendesha lenyewe usiku watu wakiwa wamelala hili ni tukio la kinyama hakujali maisha ya watu lakini hakujali hata gharama za mtambo huu, mgodi unamilikiwa na Serikali na mwekezaji ni kodi za Watanzania ziko hapa”amesema Komba.
Kufuatia tukio hilo watu wawili waliokuwa wakinunua mafuta kutoka kwenye mtambo huo wamekamatwa na Jeshi la Polisi limetakiwa kuhakikisha wanamtafuta na kumkamata aliyekuwa akiendesha mtambo huo ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake,
Aidha kikao cha kamati ya ulinzi na usalama kilichokaa na uongozi wa Bucreef kimeutaka mgodi huo kujenga upya nyumba za wakazi hao, pamoja na kugharamia uharibifu wa mazao uliosababishwa na tukio hilo.
Afisa rasilimali watu kutoka Bucreef, Imelda Msuya amesema kuwa opereta wa mtambo alikua akiiba mafuta na alipogundua anafuatiliwa na walinzi alikimbia na kusababisha majanga hayo.
Kuhusu maelekezo yaliyotolewa na Serikali ya kujenga upya nyumba na kufidia mazao amesema wao kama mgodi watatekeleza yote waliyoelekezwa.
Mashuhuda waeleza
Mariam Kasandiko mkazi wa Isingiro amesema usiku akiwa amelala alisikia kitu kinanguruma na alipotoka nje ghafla aliona mtambo huo ukiparamia upande wa pili wa nyumba yake, huku watoto wake wakiwa ndani wamelala.

Mtambo uliotelekezwa na dereva ukiwa umesimama kwenye mashamba ya watu baada ya kugonga nyumba za watu na kusababisha majeruhi watano.
“Yaani hata sikuweza kuwaita wanangu ni ghafla sana lakini namshukuru Mungu upande ulioparamiwa siko walikokua wamelala, hivyo wamejeruhiwa tu na tofali na tayari wamepelekwa hospitali na wanaendelea vizuri”amesema Kasandiko.
Filipo Mhabi(13) aliyejeruhiwa maeneo ya mgongo amesema akiwa amelala alishtuka kusikia kelele na ukuta ukidondoka, ndipo kaka yao aliwaita akiwataka watoke nje haraka na walipokua wakitoka ndipo tofali ziliwajeruhi.
Majeruhi wa tukio hilo wawili wamelazwa Hospitali ya Katoro huku mama na mtoto mchanga ambao pia walijeruhiwa katika tukio hilo, wakiwa Hospitali ya Mkoa ya Geita.