
WAKATI ikibakia michezo mitano kwa ajili ya kumalizia msimu huu wa 2024-2025, timu ya African Sports imekuwa kinara wa kuruhusu mabao zaidi hadi sasa (50), ikifuatiwa na maafande wa Green Warriors (42), huku Biashara United ikiruhusu 39.
Timu nyingine zenye ukuta chujio hadi sasa ni maafande wa Transit Camp walioruhusu pia mabao 39, huku Kiluvya United na Cosmopolitan zikiruhusu 37, zikifuatiwa na Polisi Tanzania (32), Mbuni FC (29), Songea United (26) na TMA FC iliyoruhusu (23).
African Sports ni mabingwa wa Kombe la Muungano mwaka 1988, ikipanda Ligi ya Championship msimu huu baada ya kushuka daraja msimu wa 2022-2023 iliposhika nafasi ya 14 na pointi 23, huku msimu uliopita ikiwa ndio mabingwa wa First League.
Hadi sasa timu hiyo imecheza michezo 25 msimu huu ya Ligi ya Championship ambapo kati yake imeshinda minne, sare miwili na kupoteza 19, ikishika nafasi ya 14 na pointi zake 14, huku eneo la ushambuliaji likifunga mabao 21 na kuruhusu 50.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha wa African Sports, Kessy Abdallah alisema licha ya changamoto hiyo anayokabiliana nayo kwa sasa ila hilo kwake halitizami zaidi, kwani malengo yake makubwa ni kuhakikisha anaibakisha Championship msimu ujao.