
Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri amewataka Watanzania kuwekeza kupitia kituo hicho kwani kuna fursa kubwa kwao ambazo zitachochea uwekezaji wao.
Teri amebainisha hayo leo Mei 16, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akitoa semina kwa wafanyabiashara wa Kariakoo kwa lengo la kuwaonyesha fursa zilizo mbele yao endapo watawekeza kupitia TIC.
Amebainisha kwamba kuna manufaa makubwa kwa wazawa kuwekeza nchini kwa sababu kuna misamaha ya kodi wataipata katika uagizaji wa bidhaa au vifaa vinavyotumika kwenye uwekezaji wao na hivyo kuwarahisisha biashara zao.
“Kwa mfano, ukimaliza kujenga hoteli yako, vifaa vya ndani kama vile viti, vitanda, mashuka, mataulo, vimeondolewa kodi. Kwa wasafirishaji, ukiagiza kichwa cha lori, unapunguziwa import duty kwa asilimia 75 kama umepitia TIC,” amesema Teri.
Amesema ndani ya TIC kuna taasisi 16 ambazo zimewekwa pamoja ili kumrahisishia mwekezaji, baadhi ya taasisi hizo, amesema ni pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Shirika la Umeme (Tanesco), Mamlaka ya Mapato (TRA), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Wakala wa Usalama Mahali pa Kazi (Osha) na mwakilishi wa Wizara ya Ardhi.
Amewataka wafanyabiashara hasa wa Kariakoo kujenga tabia ya kuuliza ili wafafanuliwe na kufunuliwa fursa nyingi ambazo hawazijui. Amewataka kutembelea kituo hicho au kupiga simu ili kujuzwa fursa wanazoweza kuzipata.
“Mlengwa wa nafuu hizi ni Mtanzania. Ni rahisi zaidi kwa Mtanzania kuwa mwekezaji kuliko mgeni. Mtanzania unatakiwa kuwa na mtaji wa Dola za Marekani 50,000 tu, lakini mgeni anatajkiwa kuwa mtaji wa dola 500, 000,” amesema.
Teri amesisitiza kwamba sekta ya viwanda ni muhimu zaidi kwa uwekezaji kutokana na manufaa yake kwa wawekezaji na kwamba mwaka jana miradi 901 ya uwekezaji, kati ya hiyo, 400 ilikuwa ya viwanda.
Amesema katika viwanda vilivyoanzishwa, vingi vilikuwa vya uzalishaji wa vifaa vya ujenzi kama saruji, nondo, bati na misumari, uzalishaji wa vyakula, vifaa vya majumbani, nguo na samani za ndani.
“Ushauri wangu, kama unaweza kujenga kiwanda anza sasa, wekeza kwenye maeneo hayo. Ukianzisha kiwanda leo, vyuma vya kujengea na mashine havitozwi kodi,” anesema mkurugenzi huyo.
Amewataka wafanyabiashara kujisajili TIC ili waweze kunufaika na manufaa hayo na gharama za kujisajili ni dola 1,200. Ameongeza kuwa cheti cha TIC kinakaa miaka mitano, hivyo watakuwa na manufaa makubwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo, Severine Mushi amesema gharama za kujisajili za dola 1,200 (takribani Sh3 milioni) kwao ni kubwa, hivyo wameomba zipunguzwe kwa wazawa, angalau iwe Sh1 milioni.
“Tungependa gharama za usajili kwa wazawa zipunguzwe, iwe angalau Sh1 milioni ili kutoa hamasa kwa wawekezaji wazawa kwa kuwa wakizalisha, fedha zitabaki hapahapa nchini,” amesema.
Mushi ameongeza kuwa elimu waliyoipata itakwenda kuwasaidia kwani wakianzisha ushirikiano wa wafanyabiashara wa Kariakoo kwa kuunganisha mitaji, wanaweza kuwa na fedha za kutosha kuanzisha kiwanda na kufanya uwekezaji mkubwa.