
Dodoma. Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimeanza mkakati wa kujenga utamaduni wa wanafunzi kuwekeza wakiwa vyuoni, lengo likiwa ni kuongeza idadi ya wawekezaji Watanzania na kutatua changamoto ya ajira kwa vijana.
Programu hiyo inakuja wakati kukiwa na vuguvugu la vijana waliohitimu katika vyuo mbalimbali wakiwemo walimu wakipaza sauti zao za kutaka kuajiriwa na Serikali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TIC jana, katika kipindi cha kati ya Januari mwaka 2021, wamesajili jumla ya miradi 2,020 ambapo kati ya hiyo asilimia 35 inamilikiwa na Watanzania, asilimia 42.6 ni wageni huku asilimia 23.1 ni ubia kati ya Watanzania na wageni.
Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Gilead Teri amesema hayo leo Ijumaa Februari 28, 2025, wakati wa mafunzo ya programu ya Elimu ya Kifedha na Uwekezaji katika vyuo vikuu kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).
Teri amesema wanatamani kujenga kizazi kinachojua uwekezaji na kufuatilia mapema masuala ya uwekezaji wakiwa bado shuleni, ili wanapomaliza wanaanza moja kwa moja na kuwekeza.
Teri amesema takwimu zinaonyesha wawekezaji wa ndani (Watanzania) bado ni wachache na hivyo kuwafanya wa nje kuwekeza kwenye fursa ambazo Watanzania wanaweza kuwekeza.
Amewataka wanafunzi hao kuanza kukuza mitaji yao mapema ili kadri siku zinavyoenda waweze kukuza mitaji na kuwekeza, hatua ambayo itawawezesha Watanzania kumiliki uchumi wao.
Amesema lengo la programu hiyo ambayo itafanyika kwenye vyuo mbalimbali nchini ni kuwafikia wanafunzi 10,000 ifikapo mwisho wa mwaka 2025.
“Pia tunataka kuwafikia wanafunzi milioni moja ifikapo mwaka 2030, waweze kupata mafunzo kwa mara tano hadi sita kwa kila muhula,”amesema Teri.
Aidha, amesema elimu hiyo wanatarajia ifike ngazi za chini, ambapo kuna programu inayoandaliwa na kampuni za masoko ya hisa itakayowalenga vijana wadogo wa kuanzia miaka 14 hadi 26 ya kuanza kuwekeza.
Akifungua mafunzo hayo, Profesa Lughano Kusiluka amesema vijana ni mtaji mkubwa, lakini changamoto ni kukosa elimu ya uwekezaji na matumizi mazuri ya fedha.
“Fursa imekuja, tuitumie vizuri, najua kuwa mkiwekeza vizuri fedha zenu hamtakuwa mnanikwepakwepa kwenye ada,” amesema.
Amesema wanachotamani fedha kidogo wanazozipata kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) waziwekeze katika maeneo mbalimbali, ili ziweze kuzaa faida na baadaye wanaweza kuwa matajiri kwani utajiri unaanza katika miaka yao.
Naye Mhadhiri Mwandamizi katika Ndaki ya Sayansi Asilia na Hisabati kwenye chuoni hapo, Dk Lulu Kaaya amesema pamoja na jitihada zinazofanyika nchini soko la ajira limekuwa halitanuki kama inavyotakiwa.
“Hii imetufanya kuona haja ya kuingiza kitu kwa wanafunzi ambacho kitawasaidia kwenye safari ya kujiajiri na kuajiri,”amesema.
Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya kuwasaidia vijana waweze kufikia malengo yao ya Save Youth Dreams Foundation (SYDF), Dk Gloria Mheta amesema vijana watakaohudhuria semina hiyo watafahamu faida za uwekezaji na ujasiriamali.