Tiba asili zinavyoweza kuharibu figo zako

Dar es Salaam. Kama wewe ni miongoni mwa watumiaji wa tiba asili, unapaswa kujua kwamba unaziweka hatarini figo zako.

Hii ni kutokana na dawa nyingi za asili kutopitia mchakato wa kupimwa viwandani na kutoa majibu ni kiwango gani unapaswa kukitumia kujitibu, ambacho mwili unaweza kumudu au kustahimili nguvu ya dawa.

Hayo yameelezwa na daktari mbobezi wa magonjwa ya ndani na figo kutoka Hospitali ya Saifee, Mercy Julian Mwamunyi alipofanya mahojiano na Mwananchi kuhusu kambi maalumu ya matibabu itakayofanyika Jumamosi Machi 8, 2025 kuelekea siku ya figo duniani.

Kambi hiyo itakayofanyika katika viwanja vya Mwinyijuma, Mwananyamala. Kupitia kambi hiyo maalumu ya matibabu iliyoandaliwa na Manispaa ya Kinondoni kwa kushirikiana na Hospitali ya Saifee, inatarajia kupima vipimo vya awali vya figo ikiwemo mkojo na figo zinavyofanya kazi.

Figo bandia inayosaidia kuchuja damu ‘dialysis machine’ ambapo mgonjwa hutakiwa kupewa tiba ya kuchuja damu mara tatu kwa wiki mpaka atapopandikizwa figo nyingine. Picha na Khatib Mgeja.

Kwa mujibu wa Dk Mercy, tiba asili zinaleta changamoto ya figo kutokana na dawa zilizo nyingi kutopitia mchakato wa upimaji kwenye viwanda, kwani kila dawa inatakiwa iwe na kiwango ambacho mwili utaweza kustahimili.

“Ni vema ukatumia dawa kutoka kwa mtaalamu ambaye amepitishwa na Serikali na Mkemia Mkuu wa Serikali na mamlaka husika, lakini dawa ambazo hazijapimwa ni vema kuziepuka maana hujui kiwango cha ile dawa ina sumu kiasi gani, inaingia kwenye mwili na itakuletea madhara gani hapo baadaye,” amesema Dk Mercy.

Akizungumzia maadhimisho ya mwaka huu, Dk Mercy amesema watafanya kambi maalumu ya uchunguzi wa magonjwa ya figo, kupitia kauli mbiu isemayo ‘Je, figo zako ni salama? Tambua mapema, linda afya ya figo’.

“Katika kukamilisha kauli mbiu hii, Jumamosi Machi 8 viwanja vya Mwinjuma, Mwananyamala tutafanya bure vipimo vya awali tutaangalia shinikizo la juu la damu, kisukari, uzito, urefu pia tutapima mkojo kuangalia kama una shida yoyote.”

“Tutapima ufanyaji kazi wa figo kama kutakuwa na changamoto nyingine za ziada, hata kipimo cha ultrasound kitakuwepo ili kuchunguza zaidi.”

Mratibu wa tiba na magonjwa yasiyoambukiza Manispaa ya Kinondoni, Dk Omary Mwangaza amesema katika kila watu saba, mmoja ana tatizo la figo, hivyo wanataka kuwapima watu mapema wajue hali zao na kuchukua hatua.

“Hatuna kiwanda cha figo, ukianza kusafisha ni endelevu na gharama ni kubwa, Wizara ya Afya inasisitiza wananchi kujitokeza na kupata elimu namna gani ya kujiepusha na magonjwa hayo.”

“Tunatarajia kupata watu zaidi ya 1,000, tumejiandaa kuwapima bure magonjwa kama sukari, presha, figo jinsi zinavyofanya kazi, mkojo, ultrasound ya figo bure na hii inaangalia jinsi figo zilivyo, namna zilivyokaa, umbo lake likoje, jinsi zinavyofanya kazi kuendana na umri wako au zinapunguza ufanisi,” amesema Dk Mwangaza.

Amesema kwa mwaka jana walipata watu 1,200 waliojitokeza kupima na kuwapata wachache, tulianza kuwapa matibabu wasifikie hatua za kusafishwa kwa njia ya dialysis, akigusia kuongezeka kwa vitengo vya kuchuja damu inaashiria ongezeko la tatizo.

Dalili magonjwa ya figo

Akielezea dalili za ugonjwa wa figo, Dk Mercy amesema kwa sababu pia magonjwa ya figo hayajulikani dalili zake mapema, vipimo huzibaini mapema zaidi.

Mratibu wa tiba na magonjwa yasiyoambukiza Manispaa ya Kinondoni, Dk Omary Mwangaza. Picha na Khatib Mgeja.

“Kuna dalili tunazoweza kutambua mapema, mwingine akikojoa mkojo unamuwasha, unamchoma, mwingine mkojo una mapovu au kiwango cha maji alichokunywa na mkojo anaoutoa havilingani, magonjwa ya figo yanakuja kulingana na vile viashiria hatari alivyonavyo mfano sukari na shinikizo la juu la damu.”

“Mwingine hajui hali yake ya kisukari, ukimpima unakuta ipo juu unagundua na figo kumbe zilishapata changamoto siku nyingi vivyo hivyo na shinikizo la juu la damu, hivyo ni vema ukatambua figo zako mapema kama ziko salama au vinginevyo, hii itasaidia kuepuka athari mbaya hapo baadaye,” amesema.

Amesema ni muhimu kufanya uchunguzi mara kwa mara angalau mara moja au mbili kwa mwaka, hasa wale waliokutwa na changamoto awali.

Dk Mercy amesema vipimo vya awali mara nyingi havina gharama kubwa.