Thierry Henry ahofu talaka kumvuruga Guardiola

Mshambuliaji wa zamani wa Barcelona, Thierry Henry amesema kuwa kocha wake wa zamani, Pep Guardiola hayuko sawa hivi sasa baada ya kuachana na mkewe.

Guardiola amepitia nyakati ngumu katika miezi ya hivi karibuni akitalikiana na mkewe Cristina Serra na timu yake Manchester City kukumbana na kichapo cha mabao 5-1 kutoka kwa Arsenal.

Baada ya kudumu na Serra kwa miaka 30, Januari 2025, Pep aliachana na mwanamke huyo ambaye alionekana kutofurahishwa na uamuzi wa Pep kuongeza mkataba hadi 2027.

Henry ambaye mwaka 2007 naye alikutana na madai ya talaka yaliyopelekea ndoa yake kuvunjika alisema anajisikia vibaya kuhusu Guardiola.

“Najisikia vibaya kuhusu kilichomtokea Pep na Man City? Ndio najisikia kwa kitu kimoja. Sio rahisi kushughulika na anachoshughulika nacho Pep nje ya uwanja.

“Nilipitia hali hiyo wakati nilipokuwa Barcelona. Hauwezi kushughulika na vitu kama hivyo kama hali yako kiakili haiko sawa.

“Naweza kukuambia sio rahisi. Hakuna anayeweza kukabiliana na hilo wakati huo ukitakiwa kuonyesha ufanisi kila wakati. Hivyo nafikiria tunaweza kuelewa.

Kwa sasa Pep na Serra wanaishi tofauti ambapo mwanaume anaishi England na mwanamke anaishi Barcelona, Hispania akiwa na watoto aliozaa na mwanaume.