Thamani ya utamaduni inapungua

Dar es Salaam, Ni miaka 25 toka Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipofariki, nimekaa natafakari safari  ya maisha yangu ya muziki, safari iliyoanza enzi ya awamu ya kwanza ya uongozi wa nchi yetu, enzi ya awamu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mimi ni mzaliwa wa Iringa, nilipata bahati kuzaliwa katika nyumba ambayo muziki ulikuwa sehemu kubwa ya maisha.

Wazazi wangu walikulia enzi ya ukoloni, enzi hizo katika elimu, moja ya mambo yaliyotiliwa mkazo sana enzi hizo ni sanaa, shule zilifundisha mambo kadhaa ya sanaa yakiwemo muziki, baba akaweza kujifunza vyombo mbalimbali vya muziki, hatimaye nami nikafaidika kulelewa katika nyumba iliyopenda muziki.

Pamoja na lawama nyingi kuwa wakoloni walikuja kuharibu utamaduni wetu, hakika yanayofanyika sasa ndio hasa yanayofukia kabisa utamaduni wetu.

Baba yangu alikuwa mpiga gitaa mzuri aliyerekodi nyimbo zake kwa mara ya kwanza katika kituo cha redio pekee kilichokuweko wakati huo Tanganyika Broadcasting Services (TBC) mwaka 1959, alirekodi tena mwanzoni mwa mwaka 1960 na nyimbo hizo kupigwa kwa mara ya kwanza katika kipindi cha Jimbo Letu, 16 Mei 1960.

Baba alilipwa shilingi 40 na risiti bado iko. Wakati huo ungeweza kununua gari jipya kwa shilingi 800, hivyo ni wazi kiwango kilicholipwa na redio hakikuwa kidogo, ikumbukwe huo ulikuwa wakati wa ukoloni, ni ushahidi kuwa kabla ya Uhuru baadhi ya wanamuziki walikuwa wakilipwa mirabaha kwa kazi zilipotumika katika redio.

Nikiwa na umri mdogo kabisa, nilianza kushirikishwa kuimba wakati baba akipiga gitaa, na kwa kuwa nyumbani tulikuwa na radio na gramaphone iliyokuwa na santuri za muziki aina mbalimbali, muziki wa Kiswahili, Kihindi, Kiingereza na muziki toka Afrika ya Kusini, Kongo na Cuba, hivyo toka mapema masikio yangu yalizoea kupenda muziki wa aina mbalimbali.

Nilianza shule mwaka ambao Tanganyika ilipata Uhuru, nakumbuka siku moja kabla ya siku ya Uhuru, wanafunzi tulifagia barabara za jirani na shule yetu kisha kuzimwagia maji siku moja kabla ya Uhuru, ili siku ya Uhuru kusiwe na vumbi.

Baada ya Uhuru utaratibu wa enzi ya ukoloni uliendelea, shule zilikuwa na kipindi kilichoitwa ‘Kuimba’, walimu walifundisha nyimbo na kulikuwa na vitabu maalumu vya somo hilo, nyimbo katika vitabu hivyo zilizokuwa na mafunzo mbalimbali ya maisha, kuheshimu wazazi, wakubwa, kupenda shule na kadhalika, kwa ujumla maadili mema.

Somo hili lilikuweko katika ngazi zote za elimu, na kulikuweko walimu wengi waliokuwa wakijua hata kusoma na kuandika muziki kwa nota hivyo wanafunzi kupewa elimu ya muziki zaidi ya kuimba nyimbo.

Nilitamani aidha kuwa mpiga ngoma au mpiga filimbi na kubwa kuliko yote ni kupata bahati kuwa mshika fimbo. Bendi hizi za shule zilikuwa zikipiga muziki wa hali ya juu, walimu hawa waliokuwa na utaalamu wa muziki waliwezesha bendi hizi kuwa za kiwango cha juu.

Shule zilishindana kwa kuzivalisha bendi mavazi bora na upigaji kuwa makini na hivyo siku za sikukuu kila shule ilijitahidi bendi yake ndio iwe bora. Hakika nakumbuka raha iliyokuwepo wakati shule mbalimbali zilipokutana siku ya siku kuu au kukiwa na maandamano na kisha kila bendi kupita mbele ya mgeni wa heshima, wanafunzi tulijitahidi kuwa wasafi, wakakamavu na wenye nidhamu ili shule yetu ishinde. 

Kila shule ilikuwa na vikundi vya kwaya, ngoma za asili na shule nyingine zilikuwa hata na bendi za muziki wa kisasa uliotumia magitaa na vinanda. Nilisoma shule iliyokuwa na wahindi wengi, Iringa Aga Khan Primary School, bila kujali kabila wote tulicheza ngoma mbalimbali za asili.

Hakika kulikuwa na watoto wa kihindi walioweza kucheza sindimba kuliko waswahili. Siasa ya Ujamaa iliingia wakati niko darasa la saba. Mambo mengi yalibadilika, nyimbo, ngoma ngonjera, mashahiri yalianza kuwa ni ya kisiasa, nyimbo nyingi za kiasili zikapewa maneno ya kisiasa, maafisa utamaduni ndio walikuwa mstari wa mbele kuhakikisha hili, kwa kuzunguka kuhamasisha na hata kutoa adhabu kwa vikundi vilivyoonekana havitaki kuimba nyimbo za siasa.

Bendi za kigeni ambazo zilikuwa zikitunga na kuimba nyimbo kwa lugha za kwao zililazimishwa kuanza kutunga na kuimba Kiswahili. Shuleni tulianza kuimba nyimbo za siasa na za uzalendo kwa uwingi zaidi, somo la kuimba lilikuwa likifundisha nyimbo za kizalendo zaidi.

Kwaya zilizokuwa na nyimbo mbalimbali za siasa kutoka kila upande wa nchi, zilirekodiwa na Radio ya Taifa ambayo kwa wakati huu iliitwa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD). Uzalendo ulikuwa ndio ‘habari ya mjini’.

TANU Youth League (TYL) ilikuwa na matawi mpaka ngazi za vijiji na matawi haya ya TYL yalichangia sana kuendeleza muziki nchini, kwani kila kwenye tawi la TYL lazima kulikuwa na kundi la muziki aidha kwaya au ngoma, na mara nyingi vyote kwa pamoja na kuna wilaya nyingi zilikuwa na vyombo vya muziki wa dansi na Taarabu vilivyomilikiwa na  TANU Youth League, wanamuziki wengi maarufu wa miaka hiyo na ambao nyimbo zao bado maarufu mpaka leo walikotokea au walipitia bendi hizi za TYL.

Pale Iringa, vyombo vya TYL hatimaye viliishia kuwa chini ya shule ya Sekondari ya Mkwawa na hivyo pale shule hiyo kuwa na bendi nzuri sana ambayo iliweza kuja kurekodi RTD ikiwa na mtindo wao wa Ligija. Mashirika ya umma, taasisi mbalimbali za kiserikali zilihamasishwa kuwa na vikundi vya utamaduni ambavyo ndani yake kulikuwa na kwaya, bendi na ngoma za asili.

Vingi vilikuja kuwa maarufu nchi nzima, kama vile BIMA, vikundi vya majeshi yote, DDC, TANCUT, UDA, URAFIKI ana kadhalika. Pamoja na kutoa burudani vikundi hivi vilijenga uzalendo kwa vijana wa wakati ule.