
Dar es Salaam. Thamani ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) imefikia Sh748 bilioni kutoka Sh445.3 iliyokuwapo katika mwaka 2020/2021.
Thamani ya mfuko huo inatarajiwa kufikia Sh766.6 katika mwisho wa mwaka 2024/2025 wakati ambao WCF imefanikiwa kuwalipa fidia wafanyakazi na wategemezi wao wapatao 19,650 waliopata ajali, ugonjwa au kufariki wakiwa wanatimiza majukumu ya kazi zao.
Hayo yameelezwa leo Alhamisi, Mei 15, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa WCF, John Mduma katika mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari na waandishi, akielezea miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan sambamba na miaka 10 ya kuwapo kwa mfuko huo.
Mkutano huo ulifanyika jijini Dar es Salaam ikiwa ni chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Mduma amesema mbali na ukuaji wa mfuko ulioshuhudiwa pia wameboresha mifumo ya ushughulikiaji wa fidia kwa wafanyakazi kwa kutumia mifumo ya Tehama, ambapo sasa zaidi ya asilimia 90 ya huduma zinazotolewa na WCF zinapatikana mtandaoni.
“Hatua hii imeongeza ufanisi na tija katika utendaji kazi wa mfuko,” amesema mduma.
Hili linashuhudiwa wakati ambao kumefanyika mabadiliko ya kisera kwa ajili ya kuboresha huduma zinazotolewa na mfuko huo, huku moja ya eneo lililoguswa ni kushusha ada za uchangiaji katika mfuko wa watu wa sekta binafsi kutoka asilimia 1 hadi asilimia 0.5 ya mapato ya kila mwezi ya wafanyakazi wao.
“Uamuzi huu umefanya taasisi binafsi kuchangia sawa na taasisi za umma na lengo ni kumpunguzia mzigo mwajiri, ili fedha alizokuwa akitumia kuchangia sasa azielekeze kwenye maeneo mengine ya uendeshaji na uzalishaji,” amesema Mduma.
Hilo limechangia kuongeza usajili wa waajiri kwa mwaka kutoka 2,289 mwaka 2020/21 mpaka waajiri 4,136 idadi ambayo ilipelekea kufikia jumla ya waajiri 38,512 waliopo ndani ya mfuko huo sasa.
“Hii ni kutokana na hatua za makusudi za Serikali kuweka vivutio vya kufanya biashara na kuondoa vikwazo vilivyokuwepo ikiwa ni pamoja na kupunguza viwango vya uchangiaji na kutoa msamaha wa riba,” amesema Mduma.
Kwa mujibu wa Mduma, tathmini iliyofanywa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) inaonesha WCF kuwa imara kwa miaka 30 ijayo.
“Ukuaji huu unaashiria namna ambavyo WCF ilivyokuwa na utaratibu madhubuti katika usimamizi fedha na uwekezaji. Kuongezeka kwa thamani ya mfuko kunaashiria uendelevu na uhimilivu wa kutekeleza Majukumu yake.”
Mbali na hilo, WCF sasa imekuwa sehemu ambayo nchi mbalimbali zinakuja kujifunza ikiwemo Kenya, Zambia, Malawi na Ethiopia huku Namibia wakiwa mbioni kuja kuchota ujuzi huo.
Hata hivyo, kwa upande wa Afrika Kusini kila mmoja alijifunza kwa wenzake huku Tanzania ikivutiwa zaidi na matumizi ya akili mnemba katika kuendesha mfuko huo, jambo ambalo wanatamani kuliendeleza hapo baadaye.
Pamoja na mafanikio yaliyoonekana, Mduma amesema bado kumekuwa na ucheleweshaji katika kuwasilisha michango kutoka kwa baadhi ya waajiri huku baadhi ya wanufaika wakiwasilisha nyaraka pungufu.
“Pia kumekuwa na matarajio yasiyo halisi juu ya viwango vya fidia kwa baadhi ya wafanyakazi wanavyodhani wanapaswa kulipwa,” amesema Mduma.
Kuwepo kwa matarajio makubwa kumefanya baadhi ya watu waliopata ajali kazini kujaribu kutoa taarifa za uongo ili wapate fidia kubwa jambo ambalo limewahi kuwafikisha baadhi ya watu mahakamani na kuhukumiwa.
“Hadi sasa kima cha chini cha fidia kimeongezeka kutoka utaratibu wa awali ambao haukuwa na kima cha chini cha fidia kwa mfanyakazi ambaye hakupata ulemavu wa asilimia 100 hadi kufikia Sh275,333 kwa mwezi, huku kima cha juu kikiwa ni Sh8 milioni kwa mwezi kulingana na mshahara anaopokea,” amesema.
Kuhusu fidia kwa watu waliopoteza wake au waume, Mkurugenzi wa Uendeshaji WCF, Anselm Peter amesema wakati mwingine wamekuwa wakitumia hadi majirani ili kupata ushahidi kama wawili hao walikuwa wakiishi pamoja kabla ya mmoja kufariki dunia.
“Majirani wakisema wanakufahamu na mmekuwa mkiishi kama mke na mume kwa zaidi ya miaka miwili basi tutahakikisha haki yako haipotei na unastahili kulipwa fidia,” amesema Peter.
Mwakilishi wa msemaji wa Serikali, revocastus Kassimba amesema uwepo wa mikutano kama hiyo umeongeza uwajibikaji kwa taasisi za umma kutokana na kutakiwa kufanya mawasilisho mazuri, yenye tija kwa jamii mbele ya vyombo vya habari.
Mwakilishi wa Jukwaa la Wahariri (TEF) Bakari Kimwanga ameomba ushirikiano zaidi kati ya WCF na vyombo vya habari ili kuhakikisha habari nyingi zaidi zinawafikia wananchi.