Thamani iliyofichika katika taka za kielektroniki -2

Dar es Salaam. Tanzania inakabiliana na changamoto za usimamizi wa taka za kielektroniki kutokana na ukosefu wa elimu, teknolojia na miundombinu bora.

Taka hizi zenye kemikali hatarishi zina madhara kwa mazingira na afya ya binadamu.

Hata hivyo, zina thamani kiuchumi kupitia urejelezaji wa rasilimali kama shaba, plastiki na dhahabu.

Changamoto ya usimamizi

Mwenyekiti wa Mtaa wa Feri, Juma Mwingamno anasema ni jukumu lao kusimamia usafi wa mazingira.

“Taka za kieletroniki, yakiwamo mabaki ya simu kwa maelezo ya maofisa mazingira zinatakiwa kutenganishwa na si kutupwa kiholela kwa sababu ndani yake kuna vitu vinavyoweza kuleta athari kwa afya ya binadamu,” anasema Mwingamno ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wenyeviti Mkoa wa Dar es Salaam.

Anasema athari hizo pia zipo kwa viumbe vingine hai na ikolojia zake, hivyo ni lazima zitupwe kwa utaratibu maalumu.

Mwingamno anasema viongozi wanapaswa kutoa elimu ya kuhifadhi mazingira kwa umma, hasa kutenganisha taka.

Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Shimo la Udongo Kurasini, Stanley Lima anasema taka za kieletroniki zinaongezeka kwa sababu watu wengi wananunua vifaa feki.

“Mtu anaona gharama kununua kifaa kizuri akihofia kutoa fedha nyingi, unakuta kuna TV ya Sh40,000 na nyingine inauzwa Sh100,000 mtu anakimbilia inayouzwa bei rahisi matokeo yake inaharibika wanakwenda kutelekeza kwa mafundi,” anasema.

Lima anasema kuna wananchi hutupa taka za kieletroniki barabarani, mathalani televisheni zilizochoka bila kujali na wakikamatwa kiongozi anaonekana mbaya.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mbezi, Asha Voniatis anasema kukabiliana na taka za kieletroniki ni lazima wapatikane wawekezaji kama ilivyo kwenye chupa za plastiki.

“Kuwa na viwanda kutaleta tija ya usafi na kuwarahisishia watakaokuwa wanaokota na itakuwa ajira kwa waokotaji, kikubwa elimu inahitajika ili tutumie taka hizo kutengeneza vifaa vingine,” anasema Voniatis.

Pia, anasema kila taka ni mali iwapo jamii itatulia na kuitazama kama fursa.

Uzalishaji taka za kielektroniki

Kwa mujibu wa Ripoti ya Global E-Waste Monitor ya mwaka 2019, dunia ilizalisha tani milioni 53.6 za taka za kielektroniki idadi inayotarajiwa kuongezeka kwa asilimia 39 ifikapo mwaka 2030.

Kati ya taka hizo ni asilimia 17.4 pekee zilikusanywa na kurejelewa rasmi, huku asilimia 82 zikitelekezwa au kushughulikiwa isivyo sahihi, jambo linalosababisha athari kwa mazingira na afya ya binadamu.

Kwa Tanzania, Ripoti ya Taifa ya Takwimu za Taka za Kielektroniki, 2019 (NEWSR, 2019) inaonyesha vifaa vya kielektroniki (EEE) vilivyoingizwa sokoni Tanzania Bara vimeongezeka kutoka tani 21,692 mwaka 1998 hadi tani 47,504 mwaka 2017.

Ongezeko la vifaa vya kielektroniki limeongeza uzalishaji wa taka hizo kutoka takribani tani 2,000 mwaka 1998 hadi tani 35,755 mwaka 2017.

Kauli wakusanya taka

Meneja Mkuu wa Mav Recycling Limited wanaojihusisha ukusanyaji na kuchakata taka za kieletroniki, Jackline Kessy anasema kampuni hiyo iliyoanzishwa miaka mitatu iliyopita inakusanya taka zote za kieletroniki, kuzifungua, kubomoa au kuchambua kulingana na aina zake.

Akieleza namna wanavyofanya kazi akiwa kwenye ghala lililosheheni mifuko mikubwa yenye bidhaa tofauti zilizotenganishwa kwa aina anasema:

“Tunatenganisha kwa sababu kila aina ya kifaa (taka) kina kazi yake. Pia, baadhi ya bidhaa hizi ni hatari, lazima kila moja ifanyiwe kazi kulingana na ilivyo.”

Jackline anasema si bidhaa zote za taka za kielektroniki zinaweza kurejelezwa nchini.

“Mfano unaona hizi solar panel (paneli za umeme jua), tunatoa betri na vifaa vidogo vya plastiki lakini hili la juu (akionyesha mkusanyiko wa vioo) hakuna teknolojia ya kurejeleza nchini,” anasema Jackline.

Anasema taka wanazozirejeleza ni aina ya plastiki na betri zenye malighafi ya risasi ambazo huuza kwa wadau wanaoshirikiana nao.

“Vifaa visivyowezekana kurejelezwa nchini tunasafirisha nje ya nchi. Japo kampuni inafikiria kuwa na kiwanda cha urejelezaji hapahapa nchini,” anasema Jackline.

Kilomita sita kutoka makao makuu ya Wilaya ya Kisarawe kuna Kampuni ya Chilambo General Trade Limited inayojihusisha na urejelezaji wa aina mbalimbali za taka, zikiwamo za kielektroniki.

Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Gideon Chilambo anasema ameanza shughuli hiyo zaidi ya miaka 10 iliyopita, wakichakata bidhaa za kielektroniki.

Anasema wanakusanya aina zote za taka za kielektroniki kutoka kwa watu binafsi na kampuni.

“Kwa kampuni mara nyingi wanatangaza tenda, tunawania tunapata, pia watu binafsi tunapokea popote watakaposema zipo tunazifuata kwani tuna usafiri,” anasema Chilambo.

Pia,  anasema thamani ya taka inategemea makubaliano baina yao na muuzaji kwa bidhaa ambazo hazikutangazwa kwa mfumo wa tenda.

“Baada ya kuzikusanya tunazitenganisha. Hapa tunapata bidhaa kama plastiki, chuma na nyingine,” anasema Chilambo.

Anasema wana mikataba na kampuni zinazojihusisha na uchakataji ambazo huziuzia bidhaa, huku zisizowezekana kurejelezwa nchini husafirishwa nje.

Hata hivyo, anasema kuna changamoto kwa baadhi ya vifaa kama balbu, CRT monitor, paneli za umeme jua, maganda ya nyaya ambazo hazina suluhu hata nje ya nchi au ipo kwa uchache na hulazimika kugharimia kuzipeleka huko.

Changamoto zilizopo

Jackline anasema changamoto kubwa ni elimu kwa jamii.

“Sisi hatununui vifaa hivi ila tunavipokea kwa atakayetaka kutupatia, ndiyo maana tunafanya kazi na kampuni zaidi kuliko watu binafsi. Sasa unakuta mtu au kampuni inataka kukuuzia bidhaa hizo. Hili ni kinyume cha kanuni za kampuni yetu,” anasema.

Chilambo anasema kuna changamoto ya kodi akililalamikia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

“Tunalipa kodi kubwa ambazo bado haziendani na biashara tunazofanya. Ningeomba Serikali ituangalie. Sisi tupo sekta ya kutunza mazingira Serikali inatubana hasa NEMC, wana kodi kubwa,” anasema Chilambo akieleza analipia vibali zaidi ya vitano kutokana na aina ya bidhaa anazochakata.

“Nalipia NEMC kibali kimoja Sh10 milioni tofauti na vibali vya mkemia mkuu ambavyo vipo fair (nafuu),” anaeleza na kutaja changamoto nyingine ni ‘compliance’ kwenye ugawaji tenda.

Anashauri kwa tenda, hasa za Serikali wasiangalie anayetoa dau kubwa pekee bali mwenye uwezo wa kumudu kazi.

“Unampa mtu tenda, je ana uwezo wa kusafirisha, kuhifadhi, ana njia nzuri za kudispose (kuteketeza)? Tunajua watu wengi wanashinda tenda na hawana uwezo, unakuta uchafu unarudi tena kwenye mazingira,” anasema Chilambo.

Hata hivyo, Ofisa Mazingira wa NEMC, Boniface Kyaruzi anasema kwa sababu ya ukubwa wa sekta na thamani ya uwekezaji wanatoa vibali kwa kila anayetaka kuwekeza.

“Kuna wanaosafirisha, wanaobeba, wanaohifadhi na wengine, hawa wote wanapewa vibali tofauti kulingana na wanavyomudu na sekta haina watu wengi huwezi kutoa kibali kimoja pekee, ila mtu mmoja anaweza akapewa vibali vyote kama anaweza,” anasema.

Kuhusu kodi anasema thamani ya taka inaakisi ukubwa wa kodi, hata hivyo baraza linafanyia kazi maoni ya wadau.

Thamani ya taka za kielektroniki

Sera ya urejelezaji wa taka ngumu jijini Dar es Salaam ya mwaka 2020 kifungu cha 1.2 kimetaja taka hizi kuwa miongoni mwa zinazoweza kurejelezwa.

“Kurejelezwa kwa taka husaidia katika kulinda rasilimali,” inaeleza sera hiyo.

Pia, Ripoti ya The Global E-waste Monitor ya 2017 inaonyesha asilimia 20 tu ya taka za kielektroniki zinachakatwa ipasavyo, hali inayosababisha upotevu wa rasilimali muhimu kama dhahabu na madini adimu. Usimamizi bora wa taka hizi ni muhimu ili kulinda afya ya binadamu na mazingira.

Ripoti hiyo inakadiria kuwa thamani ya kiuchumi ya malighafi zinazoweza kurejeshwa kutoka kwenye taka za kielektroniki, kama dhahabu, shaba na chuma ilifikia Dola 91 bilioni za Marekani mwaka 2022, lakini ni Dola 28bilioni  pekee zilizorejeshwa kutokana na changamoto za ukusanyaji na urejelezaji.

Ripoti hiyo inasema uboreshaji wa miundombinu ya urejelezaji inaweza kusaidia kuzuia upotevu wa rasilimali na kupunguza athari za mazingira, kama vile kuokoa uzalishaji wa kilo bilioni 93 za gesi chafu kila mwaka.

Kwa mujibu wa wataalamu, uwekezaji katika usimamizi endelevu wa taka za kielektroniki na kukuza uchumi rejelezi ni muhimu ili kupunguza athari za taka hizo na kutumia rasilimali kwa njia endelevu.

“Watu wanatakiwa kujua bidhaa zinazopatikana kwenye vifaa vya kielektroni ni za viwango vya juu. Plastiki utakayopata ni ya viwango vya juu, shaba, aluminiamu au madini yoyote yanayounda vifaa hivi ni ya viwango vikubwa,” anasema Omahe Nyangi, mtaalamu wa mazingira.

Kwa nini ni taka hatari

Taka zina athari kubwa kwa mazingira na afya ya binadamu kutokana na kemikali hatarishi kama risasi, zebaki, lithium na cadmium.

 “Betri zipo aina mbili ile ya lithium na risasi ambazo zikiwekwa kwenye udongo hakuna kitu kinaweza kuota kwenye udongo huo milele. Kwa hiyo ni hatari, hapa nchini tunachakata risasi ila lithium hatuna,” anasema Chilambo.

Utafiti wa Science of the Total Environment (2012) ulibaini viwango vya juu vya metali nzito katika udongo wa maeneo ya kuchakata taka nchini Ghana, hali inayoharibu ardhi na kuchafua vyanzo vya maji.

Uchomaji wa taka hizi huzalisha sumu kama dioxins na furans zinazochafua hewa. Utafiti wa Greenpeace Research Laboratories Technical Note (2008) ulionyesha viwango vya juu vya sumu hizi kwenye maeneo ya kuchakata taka nchini China, hali inayosababisha magonjwa ya njia ya hewa.

Kwa upande wa afya, utafiti wa Environmental Health Perspectives wa mwaka 2008 ulibaini watoto wanaoishi karibu na maeneo ya kuchakata taka nchini China walikuwa na viwango vya juu vya risasi kwenye damu, hali iliyosababisha kupungua kwa uwezo wa akili na matatizo ya ukuaji.

Vilevile, utafiti wa Jarida la Afya la The Lancet Global Health wa mwaka 2013 ulionyesha ongezeko la magonjwa ya saratani ya mapafu na matatizo ya kupumua kwa wafanyakazi wa kuchakata taka kwenye nchi zinazochakata taka hizo kwa wingi.

Itaendelea kesho