Dar es Salaam. Kukosekana kwa taasisi imara zinazoyaweka pamoja makundi mbalimbali ya Waafrika kujadili kuhusu hatma ya bara lao, kimetajwa kuwa kikwazo cha kupatikana jawabu la changamoto zinazoikabili Afrika.
Kwa mujibu wa Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, zamani Afrika ilikuwa na taasisi mbalimbali za vijana, wanawake na makundi mengine zinazowaweka pamoja kujadili na kujenga hatima njema ya bara kwa ujumla wake.
Katika kulisisitiza hilo, amesema hata Umoja wa Afrika (AU) na taasisi za elimu ya juu za sasa, hazijaamua kutafuta jawabu la vikwazo mbalimbali vya kukua kwa Afrika.

Mbeki ameyasema hayo jijini Dar es Salaam jana Jumatano, Mei 21,2025, alipotoa mhadhara kwa wanafunzi na wanazuoni wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), katika hafla ya Siku ya Afrika iliyoandaliwa na Thabo Mbeki Foundation.
Katika mhadhara huo, amesema bara hilo ilikuwa na taasisi ya vijana iliyowezesha kuwakutanisha wote kama Waafrika wakajadili kutafuta jawabu la changamoto za Afrika.
Kama hiyo haitoshi, amesema kulikuwa na taasisi ya wanawake iliyotekeleza jukumu hilo kwa upande wa jinsia ya kike, lakini kwa sasa zote hizo hazipo.

Kutoweka kwa taasisi hizo, amesema kunawafanya Waafrika wakose umoja katika kutafuta suluhu ya changamoto za ajira na maendeleo yao, hatimaye mataifa ya kigeni yanafanya kwa niaba.
“Bara letu linapaswa kujitegemea na linapaswa kutafsiriwa na sisi wenyewe na sio Wachina, Wahindi, Warusi na Wamarekani,” amesema.
Amesema taasisi za Afrika ndizo zinazopaswa kutafsiri sera za bara husika na kuonyesha namna linavyopaswa kukua kiuchumi, kisiasa, ulinzi na mambo mengine.
“Bahati mbaya Waafrika hatulijui hilo na hilo ni tatizo kubwa. Rais Kikwete (Rais wa awamu ya nne wa Tanzania Jakaya Kikwete) na watu wengine wa umri wake wanapaswa kujua, tulikuwa na taasisi zinazotuweka pamoja, lakini sasa hazipo tena,” amesema.
Awali, amesema kulikuwa na harakati za vijana kuhusu umajumui wa Afrika na walikutana na kujadiliana kuhusu nini kinapaswa kufanywa kwa ajili ya Afrika.
Amesema lakini sasa hilo limepotea na hata ule umoja wa wanafunzi wa Afrika uliokuwepo na kujadiliana mambo mbalimbali kuhusu bara hilo, kwa sasa umepotea.
“Tunawezaje kupata jawabu la maswali kuhusu ajira na uwezeshaji wa vijana, ninachosema ni kwamba vijana nao wanapaswa kuwa sehemu ya watu wanaojibu swali hilo,” amesema.
Bahati mbaya, amesema hakuna taasisi inayowakutanisha vijana kuwa na nguvu ya pamoja na kutoa kauli moja kama vijana wa Afrika.
Ametaka taasisi za elimu ya juu zirudishe jukumu la kujibu maswali ya namna gani nchi za Afrika zinaweza kusimamia na kutumia uhuru zilionao.
Katika hatua nyingine, Mbeki amewataka washiriki kutafakari kuhusu umuhimu na uelewa wa sera kuu za bara, hasa zile zinazohusu maendeleo ya vijana na kuhoji ni wangapi wanazifahamu.
Amesisitiza baadhi ya kamisheni za Umoja wa Afrika (AU) hazijafanya kazi kwa ufanisi katika nchi kama Tanzania, jambo linaloonesha pengo kati ya mifumo ya taasisi na matokeo halisi kwa wananchi.
Ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa Afrika kurejesha moyo wa uwajibikaji unaosukumwa na dhamira ya kujitoa kwa ajili ya jamii, kama ilivyokuwa wakati wa harakati za ukombozi.

Kwa upande wa Kikwete amesifu maono ya Taasisi ya Thabo Mbeki ya Afrika isiyokaa kando katika maendeleo ya dunia.
“Moto wa uamsho wa Afrika umechochewa tena, na nawataka viongozi na wadau kufanya mageuzi ya kweli badala ya mabadiliko ya juu juu,” amesema.
Akizungumza katika mhadhara huo, Makamu wa Rais wa Masuala ya Uendelevu (Afrika) katika AngloGold AshantI, Simon Shayo amehoji ni kwa nini Afrika inajidharau ikijilinganisha na maeneo mengine yanayoendelea kwa kasi.
Amesisitiza haja ya kuwekeza katika maarifa na uongozi wa bara ili kufanikisha mustakabali ulioamuliwa na Waafrika wenyewe.