
Mbeya. Wananchi katika vijiji saba vilivyopo katika halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, wataondokana na adha ya kutembelea umbali mrefu kufuata huduma za kipolisi baada ya Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS) kusaidia ujenzi wa kituo cha polisi.
Wananchi katika vijiji hivyo wanalazimika kutembea umbali mrefu kutafuta vituo vya polisi kwa ajili ya masuala ya ulinzi na usalama katika maeneo yao, changamoto ambayo wameishi nayo kwa muda mrefu.
Kituo kipya cha polisi kinachojengwa katika Kata ya Igoma wilayani Mbeya, baada ya kukamilika kitahudumia vijiji vya Kimondo, Igoma, Mwanzazi, Ilungu, Ulenje, Tembela na Maendeleo.
Kutokana na kuguswa na mahitaji ya jamii hiyo, TFS imesaidia mabati 96 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha polisi kwa wananchi wa vijiji hivyo ambao wamekuwa ni washiri muhimu katika shughuli za uhifadhi wa mazingira.
Akizungumza wakati wa kupokea mabati kutoka TFS, Diwani wa Kata ya Igoma, Andrew Mwaipopo amesema kituo hicho kinachojengwa kwa nguvu za wananchi, kinategemewa zaidi kwa ajili ya ulinzi na usalama.
Amesema msaada huo wa mabati unaenda kuchochea kukamilika kwa kituo hicho na kuondoa hofu kwa wananchi kutokana na eneo hilo kuwa la kibiashara na mwingiliano mkubwa wa wananchi kutoka ndani na nje ya mkoa.
“Msaada huu utapunguza makali kwa wananchi kwa kuwa badala ya michango ya mabati haitakuwapo tena, lakini tunaenda kurejesha amani na kuruhusu shughuli za kiuchumi kufanyika vyema.
“Shamba hili la miti Kiwira limekuwa na mchango mkubwa sana kwa wananchi kwa kuwa huu umekuwa mwendelezo kusaidia shughuli za kijamii kwani katika sekta ya elimu na afya wamegusa kwa kiasi kikubwa,” amesema Mwaipopo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya hiyo, Beno Malisa amesema msaada huo utaongeza uhusiano kwa wananchi na amewaomba TFS kuendelea kutoa elimu kuhusu uhifadhi na utunzaji misitu na kuendelea kutoa huduma zilizo bora kwa wananchi.
“Eneo hili lina mwingiliano mkubwa ikiwamo kutoka Njombe, linahitaji ulinzi na usalama na niwapongeze TFS kwa msaada huu ambao unaongeza uhusiano kwa wananchi moja kwa moja,” amesema Malisa.
Mhifadhi Mkuu wa Shamba hilo, Thadeus Shirima amesema kutokana na ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi wa vijiji saba vinavyozunguka shamba hilo, wameguswa kuchangia ujenzi wa kituo hicho.
Amesema pamoja na mchango huo lakini wamekuwa wakitoa fursa za kiuchumi na ajira kwa wakazi wa maeneo ya shamba hilo na kwamba msaada huo ni kuunganisha serikali na wananchi.
“Tumekuwa tukitoa misaada mbalimbali tukianza miundombinu ya barabara, afya na elimu kwa miaka mitano mfululizo, hivyo huu ni mwendelezo wetu katika kuweka ukaribu na jamii.
“Wahifadhi na wadau wa kwanza katika hifadhi hii ni wananchi na wamekuwa karibu na sisi kutoa taarifa inapoonekana kuwapo uvunjifu wa maliasili, hivyo tunafanya kama kurudisha fadhila,” amesema mhifadhi huyo mwandamizi.
Sesilia Mwantona, mkazi wa kata ya Igoma, amesema taasisi za serikali kujitolea kuunga mkono juhudi za wananchi katika miradi ya maendeleo inaongeza uhusiano na mwamko katika kushiriki shughuli za kijamii.
“Tunaipongeza na kuishukuru TFS, Shamba la Kiwira wamekuwa pamoja na sisi kwa kuwa tunaona mchango wao kwenye shughuli za kijamii, wamegusa afya, elimu na barabara kwa kujenga madaraja,” amesema Mwantona.