
HATIMAYE viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), na wale wa Bodi ya Ligi (TPLB) wamemaliza kikao chao na wizara ya Utamaduni Sanaaa na Michezo chini ya Waziri Palamaganda Kabudi.
Kikao hiki ni maalumu kwa ajili ya kujadili mustakabali wa mchezo wa Dabi ya Kariakoo ambao uliahirishwa siku ya mechi, baada ya Simba kulalamika kuwa walizuiwa na watu waliowataja kama walinzi wa Yanga kufanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam sehemu ambayo mchezo huo ulitarajiwa kufanyika, Machi 8
Viongozi hao wakiongozwa na Rais Wallace Karia, makamu wake wawili Athuman Nyamlani na Steven Mnguto pamoja na Katibu Mkuu wa TFF Wilfred Kidao wametoka uwanjani hapo saa 1:31 usiku.
Mara baada ya kutoka viongozi hao walionekana kutawanyika kwa makundi mawili ambapo wa kwanza alikuwa Mnguto ambaye amegoma kuongea lolote akisema Rais Karia ndiye ataweza kuongea.
“Kikao kimemalizika kweli lakini siwezi kuongea lolote labda mfuateni rais wangu ndiye anayeweza kusema lolote kwenye hili,”amesema Mnguto.
Wakati Mnguto akisema hivyo, Karia naye hakuwa tayari kuzungumza akitamka neno Moja pekee:”Siongei na mtu.” kisha akapanda kwenye gari na kuondoka uwanjani hapo.
Hali hiyo imeendelea pia kwa Kidao ambaye alisema:”Jamani wasubirini wizara watasema, Mimi sipo tayari kuongea lolote nawahi kupata futari,”amesema Kidao huku naye akiingia kwenye gari na kuondoka eneo hilo.
Bado Waziri Profesa Palamagamba Kabudi na wasaidizi wake wako ndani wakiendelea na kikao chao huku kundi la mwisho la wageni wao wakiwa wameshaondoka hapa uwanja wa Benjamin Mkapa ulipokuwa unafanyika mkutano huo ambao uliwahusisha pia viongozi wa Yanga na Simba ambao waliingia kwa vipindi tofauti.