
Dar es Salaam. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeufungulia Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza baada ya kufanyiwa marekebisho.
Kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo imeeleza kuwa uwanja huo ulifungiwa kutokana na miundombinu hiyo kutofaa.
“Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) limeufungulia Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kutumika kwa michezo ya ligi baada ya kufanya marekebisho yaliyokidhi vigezo vya kikanuni na sheria za mpira wa miguu,”
“Uwanja huo uliofungiwa kutokana na miundombinu yake kutofaa kutumika kama ilivyoainishwa kwenye masharti ya kanuni ya leseni za klabu umekaguliwa na kukidhi vigezo vya kikanuni baada ya marekebisho yaliyoelekezwa kufanyika,”
“TFF inaendelea kuzikumbusha klabu kuendelea kuboresha na kutunza miundombinu ya viwanja vyao vya nyumbani kwa kushirikiana na wamiliki (kwa klabu ambazo hazimiliki viwanja), ili michezo ya ligi ichezwe kwenye viwanja bora vinavyosaidia kuongeza ushindani na thamani ya ligi.”
Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda alinukuliwa akisema kuwa Uwanja wa CCM Kirumba ulishafanyiwa marekebisho hivyo TFF waende wakautazame upya kwa kuwa anaamini upo vizuri.