TFF yafafanua sababu ya Ligi ya Wanawake kusogezwa mbele

Msimu mpya wa Ligi ya Wanawake Bara uliotarajiwa kuanza rasmi Oktoba 02, mwaka huu umesogezwa mbele hadi Oktoba 09.

Ligi hiyo inatarajiwa kushirikisha timu 10, zikiwemo nane zilizosalia Ligi Kuu msimu uliopita na mbili ambazo zilipanda daraja, Mlandizi Queens na New Heroes Queens.

Akizungumza na Mwananchi, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo, alisema maandalizi ndiyo sababu iliyofanya ligi hiyo isogezwe mbele.

“Ngao ya jamii ilitakiwa ianze Septemba hii, hivyo tumesogeza mbele kwa kuwa kuna vitu vilikuwa havijamalizika kufanyiwa kazi, hivyo ligi nayo itaanza Oktoba.”

Kwa mujibu wa ratiba mpya ya Ngao ya Jamii itaanza kuchezwa kuanzia Oktoba 02 na fainali ni Oktoba 05, huku Ligi Kuu ikitarajiwa kuanza Oktoba 09.

Awali Ngao ya Jamii ilipangwa kuanza kuchezwa Septemba 24, huku ligi ikipangwa Oktoba 02, mwaka huu.

Timu nne ambazo zitacheza Ngao ya jamii ni Simba ambao walikuwa mabingwa msimu uliopita, Yanga na JKT Queens na Ceasiaa Queens iliyomaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi msimu uliopita.