TFF yabariki uraia wa mastaa Singida BS

Dar es Salaam. Kamati ya sheria na hadhi za wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) wamethibitisha kuwa wachezaji watatu wa Singida Black Stars waliobadili uraia na kuwa Watanzania, usajili wao umepitishwa na wamepatiwa leseni za kuitumikia timu hiyo.

Mwenyekiti wa kamati ya sheria na hadhi za Wachezaji ya TFF, Said Soud amethibitisha kuwa wachezaji hao wamesajiliwa kama raia wa ndani ya nchi.

“Mamlaka husika imetoa kibali cha kuwapa uraia wachezaji hao, sisi ni nani tushindwe kuifuata na kuwasajili wachezaji hao kutokana na uraia waliopewa? Ni kweli ni wachezaji wa ndani tangu mamlaka hiyo ilipotoa taarifa,” alisema Soud.

Awali, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), Almas Kasongo alisema hawezi kulizungumzia kwa kina suala hilo, lakini wanaheshimu uamuzi wa taasisi yenye dhamana ya uraia kuwapa uraia wa Tanzania wachezaji hao.

“Hilo siwezi nikalizungumzia kwa mapana na marefu, lakini kitu ambacho naweza kukielezea kwa uhakika taasisi yenye dhamana ya uraia imetoa taarifa kwamba wachezaji wamepewa uraia. Naamini chombo kutoa taarifa hiyo siwezi kuwa na neno zaidi ya kukiamini chombo cha Serikali kwa uamuzi walioutoa,” alisema na kuongeza:

“Usajili ukishakamilika sisi (Bodi ya Ligi) ndio tunaletewa huku kwa ajili ya matumizi. Kwangu nafikiri watu wa idara ya mashindano ndio wanaweza kutoa ufafanuzi.”

Kasongo alisema kama mtendaji mkuu ni anaamini taarifa ya mamlaka yenye dhamana ya mambo ya uraia kutoa taarifa kuutaarifu umma kwamba wachezaji hao wamekuwa raia, kwa upande wake hana kipingamizi.

“Nina wajibu wa kukiamini chombo cha serikali kwamba wamefuatilia mchakato kwa usahihi na kutoa uraia kwa wachezaji hao. Lakini suala la kuwa raia na mambo ya usajili ni vitu viwili tofauti, usajili una mahitaji yake na uraia una mahitaji yake.

“Kuwa raia haikufanyi uweze kusajiliwa timu fulani kwa sababu usajili una mahitaji yake. Ukikamilisha, basi usajili utakuwa umekamilika. Ni mahitaji gani sasa wanatakiwa wakamilishe na kupeleka kwenye Idara ya Mashindano ambao wanasimamia usajili ili kupata uhakika,” alisema Kasongo.

Uthibitisho huo wa TFF na TPLB umetolewa siku moja baada Mahakama Kuu ya Tanzania masjala kuu ya Dodoma kuamuru kuitwa kortini wachezaji watatu wa Singida Black Stars, ili kujibu madai dhidi yao katika kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Wakili Peter Madeleka

Taarifa za raia hao wa kigeni kupewa uraia zilianza kujadiliwa katika mitandao ya kijamii na baadaye kuchapishwa katika vyombo vya habari ndipo Januari 23, 2025, Idara ya Uhamiaji ikajitokeza hadharani na kuthibitisha ukweli wa jambo hilo.

Katika taarifa kwa umma iliyotiwa saini na Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji (SSI), Paul Msele ilisema wachezaji hao waliomba na kupewa uraia chini ya vifungu namba 9 na 23 vya Sheria ya uraia wa Tanzania, sura ya 357.