
Tetemeko hilo kubwa la ardhi lililoikumba Myanmar Machi 28 limesababisha vifo vya watu 3,354, kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa na vyombo vya habari vya serikali Jumamosi, Aprili 5. Tetemeko hilo la ardhi lililoharibu majengo na kuharibu miundombinu nchini kote, pia limesababisha watu 4,508 kujeruhiwa na watu 220 hawajulikani walipo, kulingana na chanzo hicho.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Kulingana na makadirio ya Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu milioni tatu waliathiriwa kwa njia moja au nyingine na maafa hayo, ambayo yalikuja juu ya uharibifu wa miaka minne ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
“Uharibifu ni wa kushangaza.”
Mapigano ya miaka mingi yamesababisha uchumi na miundombinu ya nchi hiyo kuwa mbaya, na kukwamisha kwa kiasi kikubwa utoaji wa misaada ya kibinadamu.
Utawala wa kijeshi umefanya mashambulizi kadhaa dhidi ya makundi ya waasi tangu kutokea kwa tetemeko la ardhi, yakiwemo takriban 16 tangu kutangazwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano siku ya Jumatano, kulingana na Umoja wa Mataifa.
Zaidi ya juma moja baada ya tetemeko la ardhi, Wamyanmar wengi wanalazimika kulala nje, ama kwa sababu hawana makaazi tena au kwa sababu wanaogopa kwamba nyumba zao zitabomoka.
Afisa mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kutoa misaada, Tom Fletcher, amekutana na waathiriwa huko Mandalay, mji ulio karibu na kitovu hicho, siku ya Jumamosi. “Uharibifu ni wa kushangaza,” ameandika kwenye mtandao wa X. “Ulimwengu lazima uungane kwa kusaidia watu wa Myanmar,” ameongeza.
Kwa kawaida Marekani imekuwa mstari wa mbele katika misaada ya majanga ya kimataifa, lakini Rais Donald Trump amelisambaratisha shirika la misaada ya kibinadamu nchini humo.
Hapo jana, nchi hiyo ilisema kuwa inaongeza dola milioni 7 zaidi kwa msaada wa awali wa dola milioni 2 kwa Myanmar.