Tetemeko la ardhi laua 1,000 Myanmar, maelfu wajeruhiwa

Tetemeko kubwa la ardhi lenye ukubwa wa kipimo cha 7.7 lililopiga Myanmar limeleta maafa makubwa, huku idadi ya vifo ikiripotiwa kuzidi 1,000 na maelfu ya watu wengine kujeruhiwa.

Kufuatia tetemeko hilo ambalo limetokea jana Machi 28, 2025 katika mji wa Mandalay, majengo mengi yameporomoka, na miundombinu kuharibiwa huku Serikali ya kijeshi ya Myanmar ikiomba msaada wa kimataifa kukabiliana na janga hilo.\

Aidha, tetemeko hilo limefika nchini Thailand na kusababisha kuporomoka kwa jengo la ghorofa 33 lililokuwa likijengwa katika Jiji la Bangkok, ambapo watu kadhaa wamefariki dunia na wengine wengi wanahofiwa kunaswa chini ya vifusi.

Timu za uokoaji zinaendelea na juhudi za kuwaokoa waliokwama, huku changamoto za miundombinu iliyoharibika zikikwamisha harakati zao.

Mashirika ya misaada ya kimataifa yameanza kutoa msaada kwa waathirika wa tetemeko hilo, huku Umoja wa Mataifa ukitangaza msaada wa awali wa Dola 5 milioni za Marekani.

Serikali za nchi jirani, pamoja na mashirika ya kimataifa, zinahamasishwa kuongeza juhudi za kusaidia waathirika wa tetemeko hilo, hasa kwa kuzingatia hali tete ya kisiasa nchini Myanmar, inayoweza kuathiri usambazaji wa misaada kwa wahitaji.

Endelea kufuatilia Mwananchi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *