
Dodoma. Idadi ya tembo katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imeongezeka kutoka 800 hadi 1,300 katika kipindi cha miaka minne, huku simba wakifikia 188.
Aidha, uongozi wa hifadhi hiyo umewaalika Watanzania wenye sherehe mbalimbali, ikiwemo ndoa, kwenda kuzifanya ndani ya hifadhi hiyo.
Takwimu hizo zimetajwa leo Jumatatu, Machi 10, 2025, na Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Dk Elirehema Doriye, alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu mafanikio na changamoto za hifadhi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Dk Doriye amesema ongezeko hilo limetokana na udhibiti wa vitendo vya ujangili ndani ya hifadhi hiyo, ambapo kwa kipindi hicho walifanikiwa kuwakamata watu 207 waliokuwa wakijihusisha na vitendo viovu, ikiwemo uwindaji haramu.
“Ongezeko hilo linatokana na mikakati ya kiulinzi, kwani mwaka 2022 tulipoteza tembo 25 waliouawa na majangili, lakini tangu kipindi hicho hadi kufikia Desemba mwaka jana (2024), mauaji kwa wanyama hao yalikuwa sifuri,” amesema Dk Doriye.
Kwa mujibu wa muhifadhi huyo, utaratibu wa watu kufunga ndoa wakiwa ndani ya hifadhi hiyo ni mpya, lakini unalenga kuhamasisha utalii wa ndani. Akitolea mfano, amesema kuwa hivi karibuni Mtanzania mmoja alifunga ndoa akiwa ndani ya hifadhi hiyo.
Hifadhi ya Ngorongoro, yenye ukubwa wa mita za mraba 8,292, ilianzishwa mwaka 1959 kwa shughuli mseto ikiwa na wakazi 8,000 na mifugo iliyokadiriwa kufikia 261,000.
Malengo makuu ya hifadhi hiyo ni uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii, na inatajwa kuwa miongoni mwa maeneo bora ya uhifadhi duniani, ikiwa na vivutio adimu visivyopatikana kokote duniani.
Dk Doriye amesema kuwa katika eneo hilo pia idadi ya faru imeongezeka kwa asilimia 40, akiwataja faru weupe 17 waliopandikizwa kutoka Afrika Kusini na kueleza kuwa kuna matumaini watazaliana na kuongezeka zaidi.
Ameeleza mafanikio makubwa yanayopatikana ndani ya hifadhi hiyo, ikiwemo ongezeko la watalii na mapato ya Serikali, hali iliyochangia maboresho makubwa ya miundombinu, ikiwemo ujenzi wa barabara.
Kiongozi huyo amebainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2024/25 wanatarajia kuvuka malengo ya ukusanyaji mapato. Hadi Februari 2025, jumla ya watalii 803,225 walitembelea hifadhi hiyo, na kiasi cha Sh212 bilioni kilikusanywa.