
Dar es Salaam. Wakati Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ikiendelea kuhamasisha taasisi za kifedha kuja na bunifu mbalimbali zitakazowawezesha watu kukopa kirahisi na kuwaepusha na mikopo kausha damu, Benki ya Biashara Tanzania (TCB) imeitikia wito huo.
Hiyo ni baada ya benki hiyo kusaini makubaliano na teknolojia bunifu ya Ramani.io itakayowasaidia wafanyabiashara kupata mikopo kirahisi, ili waweze kuagiza shehena zao za mizigo kwa ajili ya usambazaji.
Hii itawanufaisha zaidi wafanyabiashara wa kati na wadogo ambao wanachangia asilimia 30 kwenye pato la Taifa.
Akizungumza baada ya kuja na suluhisho, Ofisa mkuu wa huduma za kidijitali na kibenki na ubunifu wa TCB, Jesse Jackson amesema sasa mchakato mzima wa kupata mkopo utafanyika kidijitali ili kurahisisha hatua hiyo.
Makubaliano hayo yaliyoingiwa leo Aprili 9, 2025 jijini Dar es Salaam pia yanalenga kuondoa baadhi ya changamoto wanazokutana nazo ikiwemo kucheleweshewa mikopo, mlolongo mrefu wa huduma za kibenki ambazo zinakwamisha kufanya biashara kwa wakati na kukosa dhamana.
Wafanyabiashara hao ambao ni waagizaji na wasambazaji wa bidhaa ikiwemo vinywaji, ujenzi, nishati na dawa wamekuwa wakikwama kutokana na changamoto hizo.
“Kuongeza ufanisi katika utoaji mikopo, mchakato utakuwa wiki moja mjasiriamali na mfanyabiashara huyu apate mkopo, shehena itatumika kama dhamana yake ili aendelee na usambazaji wa bidhaa kwa Watanzania.’’
Amesema ushirikiano huo utafanya biashara kukua zaidi, kutengeneza ajira, kuongeza wigo wa Serikali kupata mapato yake pamoja na ukuaji wa uchumi wa nchi.
“Kundi hili ambalo kila biashara 10 zilizopo Tanzania tisa ni za kati na ndogo linapata changamoto pale linapohitaji mkopo kutoka benki ili kulipia mizigo au shehena zao wanazoziagiza, kwani mchakato wa kujaza makaratasi unachukua wiki tatu hadi nne.
“Sasa baada ya ushirikiano huu watapa ndani ya wiki moja hadi mbili na biashara zao zitaendelea, kwani mchakato utafanyika kidijitali na watakuwa haraka zaidi katika biashara zao,” amesema Jackson.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Ramani.io, Iain Usiri amesema wametengeneza mfumo wa kidijitali wa kusaidia benki na taasisi nyingine kufuatilia mikopo ya wateja wao kwa muda halisi.
Ushirikiano mpya kati ya kampuni hiyo na benki ya TCB utasaidia SMEs zaidi kupata mikopo kwa urahisi. Kampuni inaleta teknolojia ya kufuatilia mikopo, huku TCB ikileta mtaji.
Aidha hatua nyingine ni kuongeza ujumuishaji wa kifedha kwa wafanyabiashara hao nchini.