Dar es Salaam. Katika jitihada zake za kuimarisha mazingira ya kazi na jamii kwa ujumla, Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC Plc) imeendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuhakikisha usalama, afya na utunzaji wa mazingira.
Kupitia mipango na mikakati ya muda mrefu, TCC Plc imewekeza katika teknolojia safi na mafunzo kuhusu umuhimu wa afya na usalama kazini kwa wafanyakazi.
Meneja wa Usalama, Afya na Mazingira (Kiwandani) wa TCC Plc, Protas Kangalawe anasema kuwa kutokana na ukweli kwamba dunia inaendelea kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo pia ni tishio mahala pa kazi, kampuni hiyo imejiweka tayari kuan¬daa mifumo ya kukabiliana na changamoto hizo kiwandani hapo.
Kangalawe anasema kuwa kampuni ina kamati ya udhibiti wa majanga ambayo kazi yake kubwa ni kutathmini matukio yasiyotarajiwa yanayotokea karibuni ambayo yanaweza kuathiri mchakato mzima wa shughuli za uendeshaji wa kampuni ikiwamo uzalishaji na mauzo. Anasema kuwa tathmini hiyo huwa inafanyika mara kwa mara.
“Pia, upo Mwongozo wa Usimamizi wa Dharura ambao tunaufuata na unatueleza namna gani tunaweza kukabiliana na kila tukio lisilotarajiwa. Mfano mzuri ni wakati wa Uviko-19, ilikuwa ni jambo geni, hivyo ilitusaidia kujipanga na kulikabili kwa haraka na hatua ile ilitusaidia kufika hapa tulipo linapokuja suala la majanga,” anaeleza Kangalawe.

Meneja wa Usalama, Afya na Mazingira (Idara ya Masoko) wa TCC Plc, Shyrose Farizal (Kulia) akipokea tuzo ya Afya na Usalama mahala pa kazi duniani. Wawili (Kushoto) ni Wafanyakazi wa TCC Plc katika maadhimisho ya Siku ya Afya na Usalama Mahala pa kazi yaliyofanyika mkoani Singida.
Mbali na jitihada hizo, anasema kuwa kama kampuni wamekuwa wakifanya juhudi za dhati za kuhama kutoka kwenye matumizi ya nishati chafuzi na kwenda kwenye nishati safi na salama.
Anasema kuwa wameanza kubadilisha magari na forklift kwenda kwenye kutumia nisha¬ti ya umeme (hybrid) huku taa za viwandani na ofisini kutumia umeme wa jua badala ya ule wa TANESCO, yote ni katika kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.
Anaeleza kuwa: “Kuweka uwiano sawa baina ya kuza¬lisha hewa chafuzi na kupunguza ni jambo gumu lakini linawezekana ukiwa na mifumo sahihi. TCC Plc ina programu bora ya kuboresha mazingira ambapo inahakikisha inapunguza uzalishaji hewa chafuzi kwa kufanya maboresho ya mitambo na vifaa vya uzal-ishaji, kuanza kutumia nishati safi katika uendeshaji wa shughuli zake na kurejesha upya taka katika matumizi kuepusha kuchafua mazingira.”
Meneja huyo anasema kuwa TCC Plc pia imekuwa mstari wa mbele katika usimamizi wa taka na hutenganisha taka hatarishi kwenye mazingira na zile zinazoweza kurejeshwa kiwandani kwa ajili ya kuchakatwa na kutumika tena.
Naye Meneja wa Usalama, Afya na Mazingira (Idara ya Masoko) wa TCC Plc, Shyrose Farizal anasema jitihada hizo za makusudi ndiyo siri kubwa ya kuendelea kutambulika kama kampuni inayozingatia kanuni za usalama na afya mahala pa kazi na Wakala wa Usalama na Afya Mahala Pa Kazi (OSHA) katika tuzo zake inazoziandaa kwa nyakati tofauti. Pia, imekuwa na rekodi bora kwenye eneo la mazingira, ikinyakua tuzo kadhaa.
Shyrose anasema kuwa usalama katika kampuni hiyo ni wajibu wa kila mtu na mizizi yake imepandwa kuanzia ngazi ya uongozi hadi kushuka kwa wafanyakazi, wote wakizungumza lugha moja katika hilo.
Kampuni imeendelea kutoa mafunzo ya kila mara, kuwakumbusha wafanyakazi kuhusu umuhimu wa usalama na afya, hususan kwa aina ya sekta kama uzalishaji, anafafanua Shyrose.

Tuzo zilizotunukiwa Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC Plc) katika maadhimisho ya siku ya Afya na Usalama mahala pa kazi, yaliyofanyika mkoani Singida.
Ili kupanda mbegu za kusimamia usalama na afya kwa wafanyakazi, mbali na mafunzo, anasema wamekuwa wakitoa motisha na kutambua wafanyakazi wanaosimamia usalama hususan kwenye matumizi ya vyombo vya moto na mitambo kiwandani hapo mwishoni mwa mwaka.
Anasema pia katika jitihada za kuendelea kuongeza motisha kwa wafanyakazi wetu, utendaji wa kiusalama kwa mwaka uliopita umekuwa ni sehemu ya mgawanyo wa bonasi zinazogawiwa kwa wafanyakazi wa kiwandani.
“Kwa miaka miwili sasa, tumeendesha kiwanda bila ya kuwa na ajali kubwa yeyote. Lakini kinachotufanya kujivunia ni utayari wa wafanyakazi wetu kuwa mabalozi wa usalama kwa wengine kwa kukumbusha wenzao wajibu wao kabla ya ajali kutokea,” anasema Meneja huyo.
Hakuishia hapo, anasema kampuni hiyo ya sigara imekuwa ikijikita katika kujenga jamii inayozingatia usalama, afya na utunzaji mazingira kwa kushiriki katika matukio mbalimbali ya utunzaji mazingira.
Kwa kushirikiana na Manispaa ya Temeke na Uongozi wa Mkoa wa Dar Es Salaam, TCC Plc imekua ikiratibu mazoezi mbali mbali ya usafi wa maz¬ingira katika maeneno tofauti tofauti ya Mkoa wa Dar Es Salaam sambamba na ugawaji wa vifaa vya usafi katika mae¬neo hayo.
“Kwa mwaka 2023 na 2024 tumeendesha zoezi la usafishaji wa fukwe za Kigamboni na Coco Beach na baada ya hapo tunachambua taka zote tulizo-kusanya papo hapo katika jamii husika ili kuonyesha uwajibikaji wetu,” anaeleza zaidi.
Kutokana na maendeleo ya mifumo ya akili mnemba (bandia), TCC Plc imeendelea kuwekeza katika mifumo ya kisasa inayoendeshwa na akili bandia ambayo inadhibiti usalama, afya na mazingira kwa ufanisi zaidi kiwandani hapo.
Shyrose anasema mbali na kutoa mafunzo kwa wafan¬yakazi, lakini mifumo hiyo inatoa ishara za vihatarishi vipya na njia za kukabiliana navyo kwa ufanisi zaidi bila ya kusa¬babisha athari.
Matumizi ya mifumo ya akili mnemba anasema ni sehemu ya kuunga mkono kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya Mahala Pa Kazi inayosema: “Mageuzi ya Usalama na Afya: Kutambua Mchango wa Akili Bandia na Dijitali Mahala Pa Kazi.”