
VIJANA 45 wanaocheza kikapu wenye umri wa miaka 16-18 wameshiriki katika kliniki ya mchujo wa kutafuta timu ya taifa ya vijana kwenye Uwanja wa Donbosco, Oysterbay, Dar es Salaam.
Kliniki hiyo iliandaliwa na Shirikisho la Kikapu Tanzania (TBF), ikiwa chini ya udhamini na ICARRe Foundation, ambapo Mwanaspoti lililokuwepo uwanjani hapo lilishuhudia vijana hao wakianza kwa kugawanywa katika makundi manne na kila kundi likiwa na kocha mmoja, lengo likiwa nji kuandaa timu ya taifa ya vijana.
Makocha Denisi Lipiki, Ismail Mbise, Mariam Kiwelo na Phineas Kahabi walishiriki kuwapika vijana na kwa kuanzia walikuwa wanaelekezwa na makocha hao jinsi ya kukimbia na mpira kwa kasi, kuurusha, kuziba nafasi ili mchezaji wa timu pinzani asikatize, kupeana pasi na baada ya hapo waliingia darasani.
Kamishina wa Mipango wa TBF, Aloyce Renatus aliliambia Mwanaspoti kwamba, mazoezi yaliyokuwa yanatolewa yalizingatia uwezo wa kila mchezaji na kwamba wale watakaoteuliwa watatangazwa baada ya kliniki kufanyika katika mikoa yote ya Tanzania.
Kamishina wa Makocha wa shirikisho hilo, Robert Manyerere alisema makocha watakuwa na wakati mgumu kuteua wachezaji.
“Wachezaji wote niliowaona viwango vyao vinalingana. Natoa ushauri kwa makocha wawe makini katika uteuzi wa wachezaji,” alisema Manyerere.
Mkurugenzi wa ICARRe Foundation, Richard Mtambo alisema mchezo wa kikapu nchini unazidi kukua ndiyo sababu iliyowafanya wawekeze nguvu.
“Pia ijulikane mpira wa kikapu siyo kitu cha kustarehesha, ni fursa rasmi. Ndiyo maana tumekubaliana uwekezaji tuanzie kwa timu za vijana,” alisema Mtambo.