Marekani. Mwanamuziki wa Pop Marekani, Taylor Swift pamoja na mpenzi wake, Travis Kelce wameamua kujifungia ndani ili kukwepa vyombo vya habari na mitandao baada ya uhusiano wao kuangazia sana kwa miaka zaidi ya miwili.
Wawili hao ambao walithibitisha penzi lao hapo Oktoba 2023, mara ya mwisho kuonekana pamoja hadharani ilikuwa Februari 10 mwaka huu walipohudhuria fainali ya Super Bowl ambapo Kendrick Lamar alitumbuiza.
Chanzo kimoja kimeiambia Us Weekly kwamba wawili hao wamechukua uamuzi huo kutokana na kile walichodai wanataka kuishi maisha ya kawaida kwa kutumia wakati mwingi pamoja na hadi sasa wameshatumia wiki saba katika mpango huo.

Hatua hiyo inakuja baada ya kumalizika kwa msimu wa Ligi ya Soka Marekani (NFL) ambayo Travis Kelce anaichezea timu ya Kansas City Chiefs tangu 2013, huku naye Taylor Swift akimaliza ziara yake, Taylor Swift: The Eras Tour.
“Walihitaji kuwa na wakati wao wenyewe, wanafanya vizuri, na bado wako pamoja sana na wanapendana. Wanachukua mapumziko ya kutoonekana mbele ya macho ya watu wengi,” chanzo cha karibu kutoka kwao kilieleza.
“Kutofanya chochote mbele ya umma ilikuwa ndoto yao ya muda mrefu,” chanzo kingine kilidokeza na kueleza kuwa wapenzi hao wamegundua kuwa wanapenda kutazama sinema na kufanya mazoezi wanapokuwa peke yao.
Inaelezwa kuwa Kelce alitumia vyema fursa zote zilizomjia baada ya kutangaza uhusiano wake na Taylor, alihudhuria vipindi kadhaa vya televisheni na kuzungumzia maisha yao ya ndani na hata kujaribu kubadili chapa yake kama nyota wa NFL.
Hata hivyo, ratiba zake zenye shughuli nyingi za kuchosha ziliwafanya watu kuhoji kama kweli anaweza kujitolea kikamilifu katika uhusiano hao na hata NFL, hivyo sasa ameamua kuchukua mapumziko kabla ya kuanza msimu mpya wa ligi.
“Alikuwa na kazi na mambo mengi sana mwaka jana, na hakucheza vizuri kama alivyotaka. Anataka kuwa na msimu mzuri na sio kuzingatia au kujikita sana katika uhusiano wake na Taylor,” chanzo kingine kilieleza.

Mwezi uliopita, Kelce alitangaza kuwa ataichezea Kansas City Chiefs msimu mwingine akiahidi kurejea akiwa bora zaidi kuliko hapo awali, huku kocha wake, Andy Reid akisema mchezaji huyo anafanya mazoezi sana nje ya kambi.
Lakini amekuwa akitenga muda kwa ajili kipindi cha Wave Sports + Entertainment, podikasti ya Heights kila Jumatano akiwa na kaka yake ila amejitenga na matumizi ya mitandao ya kijamii kwa zaidi ya mwezi mmoja na nusu sasa.
Septemba 11 mwaka uliopita baada ya Taylor kushinda tuzo ya MTV Video Music Awards (VMAs) 2024 kupitia wimbo wake, Fortnight (2024) alimshukuru Kelce kwa kuwa na mchango katika kazi hiyo tangu mwanzo hadi kufikia mafanikio hayo.
Uhusiano wa wawili hao ulikuja baada ya Taylor kuachana na mchumba wake na muigizaji kutoka Uingereza, Joe Alwyn ambaye walikuwa pamoja kwa miaka sita.
Taylor na Alwyn walikutana kwa mara ya kwanza kwenye Met Gala 2016 na walianza kuwa pamoja miezi michache baadaye.