
Mjadala kuhusu athari za wanandoa kuishi mbali umechukua sura mpya baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, kuligusia kwa uzito unaostahili.
Katika hotuba yake alipofungua kikao kazi cha wakuu wa taasisi za umma mjini Dodoma, Waziri Simbachawene ameeleza namna hali hii inavyovuruga ndoa na malezi ya watoto, huku akitoa takwimu zinazoonyesha udhaifu mkubwa katika mfumo wa uhamisho wa watumishi wa umma.
Kwa mujibu wa Simbachawene, tangu kuanza kutumika kwa mfumo wa uhamisho wa watumishi wa umma Septemba 2023 hadi Februari 20, 2025, jumla ya watumishi 21,404 waliwasilisha maombi ya uhamisho, lakini ni 2,334 pekee yaliyoidhinishwa. Hii ina maana kuwa idadi kubwa ya maombi—takribani 12,069—bado yapo kwa waajiri wakisubiri maamuzi, huku baadhi ya viongozi wa taasisi wakishindwa kushughulikia maombi hayo kwa haki na uwazi.
Tatizo hili linapaswa kushughulikiwa kwa haraka, kwani mbali na kusababisha msongo wa mawazo kwa wanandoa, linaathiri pia ustawi wa watoto wanaokosa malezi bora ya wazazi wawili.
Uzoefu unaonyesha kuwa mara nyingi wanandoa walio mbali huanza kwa kuonana mara kwa mara, lakini kadri muda unavyosonga, utaratibu huu hudhoofika. Hali hii huongeza uwezekano wa ndoa kuvunjika kutokana na vishawishi vya kutoka nje ya ndoa au kulegalega kwa mawasiliano ya kindoa.
Kuibuka kwa mjadala huu ni ishara kwamba tatizo lenyewe linafahamika na ugumu wake unajulikana kwa mamlaka husika, ambazo zikiamua zinaweza kupata suluhisho.
Tunaamini kuwa mifumo ya Serikali inapaswa kufanya kazi kwa kushirikiana kama alivyoagiza Rais Samia Suluhu Hassan, chini ya uratibu wa wizara ya Utumishi.
Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), ambao husajili ndoa, pamoja na Wizara ya Utumishi wa Umma wanapaswa kuwa na mfumo unaorahisisha uhamisho wa watumishi walio kwenye ndoa.
Haieleweki kwa nini mtumishi wa umma anapoomba uhamisho ili kuungana na mwenza wake anakumbana na urasimu mkubwa au hata upendeleo katika maamuzi ya baadhi ya maofisa utumishi.
Tunafahamu kuwa hatua chache muhimu zinahitajika kuchukuliwa ili kutatua tatizo hili. Kwanza, ni lazima kuwe na uwazi katika mfumo wa uhamisho wa watumishi wa umma ili kuepuka ucheleweshaji wa maamuzi usio na sababu za msingi. Pili, Wizara ya Utumishi wa Umma inapaswa kuanzisha utaratibu wa kipaumbele kwa watumishi walioko kwenye ndoa, ili kupunguza athari zinazotokana na wanandoa kuishi mbali.
Tatu, viongozi wa taasisi za umma wanapaswa kuzingatia ubinadamu na weledi katika kufanya maamuzi kuhusu maombi ya uhamisho, badala ya kuyapuuza au kuyapendelea kwa misingi binafsi.
Tayari Waziri Simbachawene amelitambua tatizo hili na kulizungumza kwa kina, hivyo hivyo, anatakiwa kuchukua hatua zaidi ili mabadiliko yaonekane katika eneo hilo. Hili ni tatizo linaoikabili Serikali na ndiyo inapaswa kulifanyika kazi kuondokana nalo.
Hatutaki kuona hali ikiendelea hadi pale ndoa nyingi zitakapovunjika na watoto wengi kulelewa katika mazingira yasiyo na malezi bora.
Ni wajibu wa Serikali na taasisi husika kuhakikisha kuwa wanandoa wanapewa fursa ya kuishi pamoja ili kujenga familia imara, jamii yenye maadili, na taifa lenye ustawi. Ndiyo maana tunasema ‘Tatizo limeshafahamika—ni wakati wa kutafuta suluhisho.’