
Unguja. Wakati aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Zanzibar, Charles Hilary akifariki dunia, wadau mbalimbali wa sekta ya habari waliowahi kufanya kazi naye wamesema kifo chake ni pigo kubwa kwa tasnia hiyo. Wamemkumbuka si tu kwa umahiri wake wa kitaaluma, bali pia kwa upendo, ucheshi na sauti yake ya kipekee waliyoifananisha na dhahabu.
Rais Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za pole kufuatia msiba huo, akisema amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Hilary.
“Natoa pole kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dk. Hussein Mwinyi, familia, ndugu, jamaa, marafiki na wadau wote wa sekta ya habari kwa msiba huu mkubwa,” alisema Rais Samia.
Akimkumbuka marehemu, Rais Samia alisema:
“Charles Hilary atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa wa zaidi ya miaka 40 katika kukuza na kuendeleza tasnia ya habari nchini, tangu akiwa mtangazaji wa redio hadi televisheni, na pia kwa ushauri aliokuwa akiutoa kwa waandishi chipukizi.”
Aliongeza: “Namuomba Mwenyezi Mungu aijaze familia yake subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu, na aiweke roho ya mpendwa wetu mahali pema peponi. Hakika sote ni wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea.”
Kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Zanzibar, Desemba 30, 2021 na baadaye Februari 6, 2023, kuteuliwa kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar nafasi iliyokuwa haijawahi kujazwa tangu enzi ya Serikali ya awamu ya tano, Charles alikuwa mtangazaji maarufu wa vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi.
Aliwahi kufanya kazi katika vituo mbalimbali vikiwemo Redio Tanzania (sasa TBC Taifa), Redio One, Deutsche Welle (DW), Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) na Kituo cha Azam Media.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi wa SMZ, Zena Said, Charles alifariki alfajiri ya Mei 11 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tawi la Mloganzila alikokuwa akipatiwa matibabu.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa salamu za pole kwa familia ya marehemu, ikiwataka kuwa na subira na ustahimilivu wakati wa kipindi hiki cha majonzi.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu leo Jumapili Mei 11, 2025, Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Raqey Mohamed amesema Charles alifariki dunia saa 9:20 usiku akiwa hospitalini Mloganzila alikopelekwa kwa matibabu.
Amesema mara ya mwisho kuwasiliana naye ilikuwa Ijumaa saa 2 usiku licha ya kuwa alikuwa anaumwa, hali haikuonekana kuwa mbaya kiasi hicho.
“Tulikuwa na matukio mawili ya kazi ya Rais Jumamosi. Nilijaribu kuwasiliana naye lakini haikuwezekana, tukalazimika kuendelea na shughuli kama kawaida,” amesema Raqey.
Wanavyomzungumza
Baadhi ya watangazaji waliowahi kufanya kazi na Charles ndani na nje ya nchi, wamezungumzia mchango wa nguli huyo wa tasnia ya habari kuwa si tu alikuwa mahiri katika taaluma, bali pia kwa moyo wake wa kutoa maarifa kwa wengine. Wamesema licha ya kuwa mtaalamu mwenye uzoefu mkubwa, Charles hakuwa na ubinafsi bali alisisitiza weledi na uadilifu katika kila eneo alilofanyia kazi.
Akizungumza na Mwananchi, Ivona Kamuntu aliyefanya kazi na Charles akiwa Kituo cha Azam, amesema mkongwe huyo ataendelea kukumbukwa kwa sifa kuu tatu; mtu mwenye utu na furaha mara zote, hakuwa na desturi ya kugombana na alikuwa mwadilifu mkubwa sana kazini.
“Wakati nikiwa Chief Anka na yeye akiwa Mkurugenzi wa Redio, mara nyingi alikuwa anatoka redioni na kuja TV, akanichukulia kama bosi wake licha ya cheo chake. Hii inaonesha jinsi alivyokuwa na maadili ya hali ya juu,” amesema Ivona.
Ameongeza kuwa pamoja na maadili hayo, Charles alikuwa mtu aliyekuwa makini sana na kazi.
“Alikuwa na desturi ya kupitia habari zote kabla ya kwenda hewani, hata kama ilikuwa ni habari ya dharura, hakukubali kurusha bila kuihakiki kwanza.
“Kama tukitaka kurusha habari ya dharura, alikuwa anasisitiza ifanyiwe marekebisho kwanza. Hakuwa tayari kufanya kosa akiwa hewani. Alikuwa ni mtu wa viwango vya juu sana kitaaluma,” Ivona ameeleza kwa hisia.
Amesema Charles pia alikuwa rafiki nje ya kazi, mtu wa kuaminika na wa kukusanya watu kama familia. “Kwa kweli tutamkosa sana. Tumepoteza mtu adhimu aliyekuwa na mapenzi ya kweli na kazi yake. Sauti yake ilikuwa zaidi ya dhahabu,” amesema kwa masikitiko.
Kwa upande wake, Abubakar Liongo aliyefanya naye kazi Redio Tanzania mwaka 1991, amesema ndiye aliyempokea na kumfundisha kutangaza mpira na kusoma taarifa ya habari na baadaye akahamia Redio One, ambapo alimfuata huko.
“Baadaye, Charles alinishawishi nihamie Redio One baada ya kuniombea kwa baba yake. Alikuwa kaimu Mkurugenzi kipindi hicho kabla ya kwenda Sauti ya Ujerumani (DW), na mimi nikaanzisha Redio Uhuru,” amesema Liongo.
Ameongeza kuwa alipoondoka DW kwenda BBC, (Liongo) ndiye alichukua nafasi yake katika kituo hicho.
“Tumefanya kazi kwa ukaribu sana. Charles alikuwa kaka yangu, rafiki yangu na mwalimu wangu. Alikuwa mchangamfu, mnyenyekevu na aliye tayari kutoa maarifa yake kwa wengine bila ubaguzi,” amesema.
Amesema Charles alikuwa mtangazaji mahiri aliyeiweka taaluma mbele, na kwamba tasnia ya habari imepoteza mtu muhimu sana.
“Tumepigwa na pigo kubwa. Yapasa kutambua kuwa tumempoteza mmoja wa watu bora kabisa waliowahi kulitumikia taifa kupitia vyombo vya habari,” amesema Liongo kwa huzuni.