
Dar es Salaam. Ili kuboresha mtandao wa barabara za vijijini na mijini, Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) unatumia mbinu mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa madaraja ya mawe, ambapo gharama yake ni nafuu, ikiokoa hadi asilimia 80 ya gharama.
Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi, Machi 20, 2025, na Mhandisi Mshauri wa Tarura, Phares Ngeleja, katika mkutano wa wadau wa usafiri na usafirishaji, jijini Dar es Salaam.
Mhandisi Ngeleja amesema Tarura ilianza kutumia teknolojia ya mawe mwaka 2017/2018 na hadi sasa madaraja 401 yamejengwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara hadi kufikia Februari 2025.
Aidha, amesema kuwa kilomita 28.92 za madaraja zimejengwa katika mikoa ya Mwanza, Kigoma, Rukwa, na Morogoro, ambayo yanatarajiwa kudumu kwa zaidi ya miaka 100.
“Katika ujenzi wa madaraja ya mawe, tunatumia rasilimali za ndani na gharama za ujenzi ni nafuu (gharama ni mara tano hadi sita chini ya daraja la saruji),” amesema.
Kwa upande wa barabara, Mhandisi Ngeleja amesema hudhibiti mwendo wa magari hadi kufikia kilomita 40 kwa saa, hudumu kwa muda mrefu bila ya matengenezo makubwa, na hata zikiharibika ni rahisi kuzitengeneza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa asasi ya Tanzania Forum Group (TFG), Injinia Abdul Awadh, amesema lengo la mkutano huo ni kujadili namna ya kutatua matatizo ya usafiri na uchukuzi kwa wananchi hasa wa vijijini.
“Tunahamasisha wahusika na wadau kuboresha miundombinu vijijini ili kuepuka changamoto hii. Vijijini, wananchi wanakutana na matatizo makubwa ya usafiri kwa sababu barabara hazipatikani, gari hazipiti, na hivyo wanakuwa na changamoto ya kutembea kwa miguu kwa mwendo mrefu kutafuta mahitaji yao muhimu kama kuni, maji, na kwenda hospitali.
“Hivyo, muda mwingi ambao wangeutumia katika shughuli za uzalishaji mali, wanatumia kutafuta mahitaji hayo na kubeba vitu vizito kwa mwendo mrefu,” amesema.
Amesema kutokana na hali hiyo, ni muhimu kwa Serikali na wadau kutembelea maeneo hayo na kuona njia bora ya kuboresha huduma mbalimbali muhimu kwa wananchi.
Katibu Mkuu wa asasi hiyo, Nelly Mtaki, amesema uboreshwaji wa miundombinu maeneo ya vijijini utaleta ahueni kwa wanawake ambao wanalazimika kubeba mizigo wakitoa kuvuna mazao, au kubeba watoto kuwapeleka hospitali.