TIMU ya Taifa ya Riadha ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), imetwaa ubingwa wa kilomita 10 upande wa wanaume katika mashindano ya mbio za nyika za majeshi ubingwa wa dunia majira ya baridi ambazo zinamalizika leo Jumamosi nchini Uswisi.
Mashindano hayo yalianza Machi 23, mwaka huu kwa kushirikisha zaidi ya wanariadha 1500 kutoka majeshi ya nchi tofuati ambapo Tanzania iliwakilishwa na wakimbiaji 10, wanawake watano idadi sawa na wanaume chini ya kocha bora wa taifa msimu uliopita, Antony Mwingereza.

Wachezaji hao walikuwa wa mbio za kilomita 10 wanaume, nane upande wa wanawake na nane ule wa wanaume na wanawake katika mbio za kupokezana vijiti mchanganyiko (mixed relay), ambapo Tanzania imetwaa ubingwa wa kilomita 10 wanaume kwa matokeo ya jumla katika mbio hizo ambazo kila nchi ilitoa washiriki watatu baada ya nyota wake Joseph Panga kumaliza wa pili na kupata medali ya fedha, lakini pia kuingiza wachezaji wengi bora (10).
Nyota hao ambao walihakikisha bendera ya nchi inapeperushwa vyema ni wanariadha wa kimataifa Joseph Panga, Inyasi Sule na Mathayo Sombi. Tanzania pia imemaliza nafasi ya tatu katika kilomita nane wanawake nyuma ya Ufaransa iliyoshika nafasi ya pili na Bahrain iliyoshika ile ya kwanza baada ya nyota Watanzania Jackline Sakilu, Magdalena Shauri na Agnes Protas kufanya kweli.

Kwa upande wa mbio za vijiti mchanganyiko wanaume na wanawake za kilomita nane Tanzania ilimaliza katika nafasi ya sita matokeo ambayo yameifanya kukusanya medali tatu katika mbio hizo, ambapo moja ni ya Dhahabu kwa matokeo ya jumla ushindi wa kilomita 10 wanaume, ya Shaba nafasi ya tatu katika kilomita nane wanawake na ya fedha ambayo alipata Panga baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye kilomita 10 wanaume kwa mchezaji binafsi.
Akizungumza na Mwanaspoti kutoka nchini Uswisi, kocha wa timu hiyo, Mwingereza amewapongeza wachezaji kwa kupambana ili kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania.
“Ushindani ulikuwa mkubwa, vijana wamepambana sana kuhakikisha wanarudi na medali, lakini pia heshima ya nchi inalindwa,” amesema Mwingereza.

Kwa upande wake mwanariadha Jackline amesema licha ya changamoto ya ugumu wa njia ambayo walikutana nayo, lakini walipambana kuhakikisha medali inapatikana. Timu hiyo inatazamiwa kurejea nchini kesho Jumapili.