Tanzania yataja ongezeko shinikizo la juu la damu

Dar es Salaam. Wizara ya Afya nchini Tanzania imesema miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza, shinikizo la juu la damu ndilo linaongoza kwa idadi ya wagonjwa wanaopata matibabu katika vituo vya afya nchini.

Kufuatia hali hiyo, Serikali imepanga mikakati mbalimbali pamoja na kuboresha miundombinu, vifaa tiba na mafunzo kwa watoa huduma za afya kwa kuwajengea uwezo watoa huduma 2,400 katika vituo 600.

Hayo yameelezwa katika taarifa iliyotolewa kwa umma leo Jumamosi, Mei 17, 2025 na Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel kuhusu maadhimisho ya siku ya kimataifa ya shinikizo la juu la damu duniani.

Amesema takwimu kutoka Mfumo wa Ukusanyaji wa Taarifa za Afya Nchini (DHIS2) zinaonyesha ongezeko la wagonjwa kutoka 1,315,000 mwaka 2019/2020 hadi 1,665,019 mwaka 2023/2024.

“Miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza, shinikizo la juu la damu ndilo linaongoza kwa idadi ya wagonjwa wanaopata matibabu katika vituo vya afya.

“Katika kipindi cha Septemba 2015 hadi Aprili 2023, kati ya wagonjwa 619,102 waliotibiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), asilimia 66 walikuwa na shinikizo la juu la damu, sawa na watu 6 kati ya 10,” amesema.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), vifo vingi vinavyotokana na shinikizo la juu la damu hutokea kati ya umri wa miaka 39 hadi 79 ambapo takribani asilimia 33 ya vifo vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza husababishwa na hali hiyo.

Kwa mujibu wa Dk Mollel, katika wiki ya magonjwa yasiyoambukiza iliyofanyika Dodoma Novemba 2024, jumla ya watu 251,557 walipimwa shinikizo la damu, ambapo asilimia 4 waligundulika kuwa na ugonjwa huo kwa mara ya kwanza.

Amesema ili kupambana na changamoto hiyo, Serikali inatekeleza Sera ya Afya ya mwaka 2007 kwa lengo la kuboresha huduma za magonjwa yasiyoambukiza, likiwemo shinikizo la juu la damu.

Amesema huduma hizo hutolewa kuanzia ngazi ya zahanati hadi hospitali za rufaa.

“Serikali imeboresha miundombinu, vifaa tiba na imekuwa ikitoa mafunzo kwa watoa huduma za afya. Kupitia Wizara ya Afya, lengo ni kuwajengea uwezo watoa huduma 2,400 katika vituo 600. Kufikia Juni 2023, watoa huduma 1,972 kutoka mikoa 19 kati ya 26 walikuwa wamepatiwa mafunzo, sambamba na ugawaji wa vifaa vya uchunguzi wa awali,” amesema.

Amesema juhudi zinaendelea kufanywa ili kuimarisha afua za kinga kwa magonjwa haya, kwa kuwekeza kwenye uhamasishaji wa mabadiliko ya mtindo wa maisha.

Amesema wananchi wanahimizwa kufanya mazoezi mara kwa mara, kuepuka tabia bwete, kuacha matumizi ya tumbaku na pombe, na kupunguza matumizi ya chumvi na vyakula vyenye mafuta mengi.

Amesema kwa waliothibitishwa kuwa na shinikizo la juu la damu, ni muhimu kufuata matibabu kwa usahihi ili kuepuka madhara zaidi.

“Wizara ya Afya inatambua na kuthamini mchango wa wadau wote wakiwemo viongozi wa dini, taasisi za kijamii, waandishi wa habari, na mashirika ya maendeleo katika jitihada za kupambana na shinikizo la juu la damu.

“Ushirikiano huu utaendelea ili kufikia jamii kwa ufanisi zaidi. Kwa pamoja, jamii inakumbushwa kuthamini afya na kuchukua hatua za kinga. Kupima shinikizo la damu kwa usahihi, kulidhibiti na kufuata ushauri wa kitabibu ni njia bora ya kuishi kwa muda mrefu,” amesema.

Hata hivyo, wataalamu wa afya wamesema wagonjwa wengi wenye shinikizo la juu la damu hawajitambui.

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo Taasisi ya Moyo wa Jakaya Kikwete (JKCI), Tulizo Shemu amesema kati ya watu wazima 10, watatu mpaka watano wana shinikizo la juu la damu na zaidi ya asilimia 60 hawatambui hali zao.

“Shinikizo la damu lina madhara, husababisha kupata kiharusi, figo kushindwa kufanya kazi, mshtuko na vifo vya ghafla, kupumua kwa shida na kuvimba miguu, macho kutoona, kifafa cha mimba na kupoteza ujauzito,” amesema Dk Tulizo.

Wataalamu wameeleza zaidi shinikizo la juu la damu lisilodhibitiwa, limekuwa likisababisha vifo vya ghafla huku wengi wao wakipata kiharusi.

Leo Mei 17, dunia inaadhimisha siku hii

Ikiwa na kaulimbiu inayolenga kuongeza utambuzi sahihi wa hali hiyo, kuzingatia ushauri wa kitaalamu, na kuhakikisha matibabu stahiki kwa wale waliogundulika kuwa na ugonjwa huo inayosema “Pima Shinikizo la Damu Kwa Usahihi, Idhibiti, Ishi kwa Muda Mrefu.”

Shinikizo la juu la damu ni hali ya msukumo mkubwa wa damu kwenye mishipa kwa muda mrefu, hali inayolazimisha moyo kufanya kazi kupita kiasi.

Sababu kuu ni pamoja na mtindo usiofaa wa maisha kama kutofanya mazoezi, ulaji wa chumvi na vyakula vyenye mafuta kwa wingi, uvutaji wa sigara, na unywaji wa pombe. Shinikizo la damu lisilodhibitiwa, husababisha magonjwa ya moyo, figo na kiharusi.

Mara nyingi hali hii haina dalili, ingawa baadhi ya watu hupata maumivu ya kichwa, kizunguzungu, kuchanganyikiwa au maumivu ya kifua.

Hivyo, inapendekezwa kupima mara kwa mara ili kubaini hali ya afya mapema kabla ya madhara kujitokeza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *