
Dodoma. Mbunge wa Mlalo(CCM), Rashid Shangazi ameitaka Serikali kueleza fursa zitakazopatikana kwa Watanzania mmoja mmoja na vikundi kupitia fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027 zitakazofanyika Kenya, Uganda na Tanzania.
Akijibu swali hilo,bungeni leo Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma amesema kupitia mashindano haya fursa mbalimbali zitapatikana zikiwemo ajira kupitia ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya michezo itakayotumika wakati wa mashindano hayo.
Ametaja fursa nyingine ni uuzaji wa vifaa vya ujenzi, kuongezeka kwa mapato katika biashara mbalimbali kutokana na matumizi kwa wageni na wadau watakaoingia nchini kushuhudia mashindano.
Nyingine ni kuongezeka kwa mapato katika huduma za jamii kama vile hoteli, nyumba za kulala wageni, migahawa, usafirishaji na huduma nyingine.
“Fainali hizi pia ni fursa kwa wachezaji wa Kitanzania kuonyesha vipaji vyao kwa mawakala wa klabu vya kimataifa,” alisema Mwinjuma.
Aidha, amesema mashindano hayo yatawezesha vikundi vya sanaa na utamaduni kujitangaza hivyo, kutangaza utamaduni wa Tanzania.