
Dodoma. Serikali imetaja faida nne zitakazopatikana kwa Tanzania kushiriki maonesho ya biashara ya EXPO yatakayoanza Aprili 12 hadi Oktoba 13 katika Kisiwa cha Yumeshima kilichopo Osaka nchini Japan.
Katika maonesho yaliyofanyika kuanzia Oktoba 1 mwaka 2021 hadi Machi 31 mwaka 2022 Dubai, Tanzania iliwezesha kusainiwa kwa hati za makubaliano 36 zenye thamani ya Sh18.5 trilioni na zilizotarajiwa kuzalisha ajira ya takribani watu 214, 5754, zilisainiwa.
Akizungumza leo Jumanne, Aprili 8, 2025, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo amesema katika maonesho ya mwaka 2025, Tanzania inatarajia matokeo makubwa katika kuimarisha taarifa za biashara zinazowezesha nchi kujipanga na kuzitambua fursa za masoko na biashara.
Ametaja faida nyingine ni kuimarika kwa uchumi wa nchi kutokana na matarajio ya kufanikiwa kupata wadau wa miradi mbalimbali ya kimkakati na ongezeko la ajira kutokana na kuendelea kwa miradi hiyo.
Dk Jafo amesema faida nyingine inayotarajiwa kupatikana ni ustawi wa jamii ya Watanzania na kusainiwa kwa mikataba ya kibiashara na uwekezaji.
“Ufunguzi wa maonesho hayo unatarajiwa kufanyika Aprili 12, 2025 na yanatarajiwa kuwa na watembeleaji milioni 28.2 kati ya hawa watembeleaji milioni 3.5 watatoka nje ya Japan,”amesema.
Aidha, amesema katika maonesho hayo Tanzania kuna siku ya kitaifa ambayo siku ya Tanzania imepangwa kufanyika Mei 25 mwaka huu, mgeni rasmi atakuwa ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Pia, amesema kutakuwa na kongamano la biashara, uwekezaji na utalii litakalofanyika Mei 26,2025.
“Serikali inatoa wito kwa taasisi za umma, mashirika ya kimataifa pamoja na mashirika binafsi kuunga mkono na kushiriki katika maonesho haya muhimu ili kuchagiza uchumi kupitia biashara, teknolojia, utalii na uwekezaji na diplomasia kwa manufaa ya nchi yetu,”amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), Latifa Khamis amesema ushiriki wa Tanzania kwenye maonesho hayo umejikita katika kutangaza fursa mbalimbali zilizopo nchini kwenye sekta za kipaumbele ikiwamo afya, nishati, madini, utalii, kilimo, uchumi wa buluu, sanaa na utamaduni.