Tanzania yapania taji Kwibuka T20

TIMU ya taifa ya Kriketi ya Wanawake imewasili, Rwanda tayari kwa michuano ya kriketi ya mizunguko 20 ijulikanayo kama Kwibuka Women T20 inayoanza kesho Jumanne jijini Kigali, ikitarajiwa kufikia tamati Juni 14.

Ni mashindano maalum ya kukumbuka miaka 31 tangu Mauaji ya Kimbari  ya Rwanda yaliyotokea mwaka 1994, ambapo nchi nyingine zinazoshiriki ni Brazil, Cameroon, Malawi, Nigeria, Sierra Leone, Uganda, Zimbabwe  na wenyeji Rwanda.

Uganda ndio watetezi  baada ya kushinda michuano ya mwaka jana na timu hiyo ya Tanzania iliyoagwa wikiendi iliyopita inaongozwa na kocha mkuu Imran Nackerdien, akisaidiwa na Rijali Fentu na mlezi Monica Paschal.

Mchezaji tegemeo wa timu na mkongwe ni Fatuma Kibasu, ambaye amekuwa kinara katika michuano mingi ya kimataifa, akiwa na imani Tanzania itashinda tena safari hii kama ilivyofanya michuano miwili ya awali.

“Tuko vizuri na tuna ari ya ushindi,” alisema.

Kibasu atakuwa akishirikiana na Doriss Kamunya pamoja na wachezaji Tabu Saidi, Sophia Frank, Shufaa Hamza, Sheila Kizito, Saum Mtae, Saum Deo na Neema Justine.

Wengine katika msafara wa timu ya Tanzania ni Nasra Nassoro, Mwanamvua Hamisi, Lina Justine, Jennifer Gabriel, Hudaa Mrisho, Getruda Mushi na Agness Qwelle

“Wachezaji wote wameondoka na ari ya kulitumikia vyema taifa la Tanzania, hivyo sisi Chama cha Kriketi tunawaomba Watanzania wawaunge mkono na kuwatakia mafanikio vijana wetu katika safari yao,” mwenyekiti wa TCA, Balakrishna Sreekumar, alisema kupitia mtandao wa Facebook.

Tanzania imeshiriki katika mashindano ya Kwibuka Memorial Women T20 mara mbili na mara zote imeshinda.

Kenya ambayo imeshiriki katika mashindano haya mara saba, imeshinda mara 4.

Watetezi Uganda wanaoshiriki kwa mara ya tisa, wameshinda ubingwa mara 3 na kushika nafasi ya pili mara 5.

Wenyeji wa mchuano Rwanda wameshiriki mara zote 10, wameshinda mara 1 na kumaliza katika nafasi ya pili mara mbili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *