
Dar es Salaam. Wakati Shirika la Afya Duniani (WHO) likipunguza idara zake kutoka 76 hadi 34 na gharama za wafanyakazi kwa asilimia 25 baada ya ufadhili kupungua, Tanzania imeanza kujipanga kukabiliana na hatua hiyo.
WHO imechukua hatua hiyo ikiwa takribani miezi minne baada ya Marekani kutangaza kujiondoa katika shirika hilo na kusitisha ufadhili wake.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Ghebreyesus, katika hotuba ya ufunguzi wa mkutano wa 42 wa Kamati ya Mipango, Bajeti na Utawala ya Bodi ya Utendaji ya shirika hilo uliofanyika Mei 14, 2025, alisema kukosa ufadhili wa Marekani na kupungua kwa misaada rasmi ya maendeleo kutoka kwa baadhi ya nchi nyingine, kunasababisha pengo la mishahara kwa kipindi kijacho cha miaka miwili (2026–2027), la zaidi ya Dola za Marekani 500 milioni.
“Ukweli mchungu ni kwamba tunahitaji kupunguza matumizi ya mishahara kwa asilimia 25. Hii haimaanishi kuwa tutapunguza asilimia 25 ya wafanyakazi katika shirika lote.
“Lakini tusijidanganye; tunawaaga idadi kubwa ya wafanyakazi walio na uzoefu, uwezo na kujitolea kwa kiwango cha juu. Hii ina maana kuwa taaluma zinakatizwa na maisha kuvurugika,” alisema.
Alisema ili kuwasaidia wafanyakazi katika kipindi hicho kigumu, wameanzisha mifumo ya msaada na kujikita kusaidia katika afya ya akili na ustawi wao.
“Tunatarajia kupunguzwa wafanyakazi wengi kutatokea makao makuu, ingawa ofisi za kanda pia zitaathirika kwa viwango tofauti,” alisema.
Alisema kazi ya kuweka vipaumbele imechangia kuandaliwa kwa muundo mpya wa makao makuu, ambao aliutangaza mwezi uliopita unaopunguza idadi ya viongozi wakuu kutoka 14 hadi 7 na idadi ya idara kutoka 76 hadi 34.
“Ofisi za kanda zinakamilisha mipango yao ambayo inaendana na makao makuu,” alisema.
Wadau wa masuala ya afya nchini, wamesema kujiondoa kwa Marekani WHO ni pigo kubwa kwa mataifa yanayoendelea, ikiwamo Tanzania na nchi maskini.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko amesema suala hilo lilitarajiwa kutokea kutokana na mwenendo wa uchangiaji WHO unaofanywa na nchi wanachama.
Amesema mchangiaji mkubwa alikuwa Marekani kwa kipindi kirefu, akifuatiwa na mashirika mengine ya China, nchi za Ulaya na Japan.
Kujitoa imechangia kupungua kwa uendeshaji wa shirika, hivyo wamefanya uamuzi kuona wanawezaje kufanya kazi kwa hali ilivyo.
“Shirika litaweza kujiendesha bila kutegemea michango mingi, litaweza kufikiri vyanzo vipya vya mapato kuchangia shughuli zake bila kukwama,” amesema na kuongeza:
“Tunajua watu wamepoteza ajira, sijajua Watanzania wangapi walikuwapo kwenye orodha ya ajira na wangapi watakuwa wameathirika kwa kupunguza kazi. Lakini pia kuna miradi iliyoendeshwa na WHO itaathirika kwa namna moja ama nyingine au kutotimiza miradi na matokeo yaliyotarajiwa kwa wanufaika wa ufadhili huo. Zipo athari lakini kwa kiasi kikubwa wamepunguza gharama za uendeshaji.” Mwenyekiti wa Chama cha watoa huduma za afya binafsi Tanzania (Aphfta), Dk Egina Makwabe amesema Marekani inachangia asilimia 30 ya bajeti ya WHO.
“Ukiangalia upande wa chanjo pale Gavi (Shirika la kimataifa linalozalisha chanjo) ule mpango wa kutoa chanjo kwa nchi maskini Marekani ndiyo ilikuwa mchangiaji mkubwa,” amesema.
Inachofanya Tanzania
Serikali ya Tanzania imesema ina akiba ya kutosha ya dawa na chanjo lakini inakuja na mikakati mipya.
“Hatuna changamoto ya ARV, hali yetu ya dawa ni nzuri na inatupeleka mpaka Juni 2026. Itakaposomwa bajeti ya Wizara (Afya) utasikia mipango ya Serikali,” amesema Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi alipozungumza na Mwananchi kuhusu mikakati iliyopo.
Uamuzi wa Trump
Rais Donald Trump wa Marekani Januari 20, 2025 alitia saini amri ya kiutendaji kujiondoa WHO, shirika lililoanzishwa mwaka 1948 likiwa na nchi wanachama 193. Marekani ilikuwa miongoni mwa waasisi.
Trump katika amri hiyo alisema Marekani itasitisha kutoa fedha, usaidizi au rasilimali za Serikali ya Marekani kwa WHO.
Taifa hilo limekuwa likitoa fedha, nyingi na watalaamu wa afya kwa kutumia taasisi zake za Serikali.
Kwa mujibu wa takwimu za WHO, Marekani katika kipindi cha mwaka 2022 hadi 2023 imetoa Sh3.25 trilioni.
Taifa hilo limekuwa likitoa wataalamu na ujuzi kupitia taasisi zake kama vile idara ya afya na huduma za binadamu, Kituo cha Kudhibiti Maradhi cha Marekani (CDC), Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), Shirika la Kulinda Mazingira la Marekani (EPA) na Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na (PEPFAR).
Wachangiaji wengine wakubwa wa WHO kwa mwaka 2022-2023 ni Ujerumani Sh2.16 trilioni, Gates Foundation (Sh2.10 trilioni), Gavi (Sh1.21 trilioni), Kamisheni ya Ulaya (Sh1.18 trilioni), Uingereza na Northern Ireland (Sh1 trilioni).
Wengine ni Canada (Sh516.46 bilioni), Rotary International (Sh448.1 bilioni), Japan (Sh422.79 bilioni) na Ufaransa (Sh407.6 bilioni).
Awali, Marekani ilipendekeza kujiondoa kutoka WHO mwaka 2020 kwa sababu ya shirika hilo kushughulikia vibaya janga la Uviko-19 lililoibuka kutoka Wuhan, China na shida nyingine za kiafya duniani.
Trump katika muhula wake wa kwanza wa Urais, aliilalamikia WHO kushindwa kupitisha mageuzi yanayohitajika haraka na kutokuwa na uwezo wa kuonyesha uhuru kutoka kwa ushawishi usiofaa wa kisiasa wa nchi wanachama wa shirika hilo.
“WHO inaendelea kudai malipo yenye kutaabisha isivyo haki kutoka Marekani, mbali na uwiano na malipo yaliyotathiminiwa ya nchi nyingine. China yenye idadi ya watu bilioni 1.4 ina asilimia 300 ya wakazi wa Marekani, lakini inachangia karibu chini ya asilimia 90 ya WHO,” alisema Trump.
Alisema Marekani inakusudia kujiondoa kutoka WHO ambapo barua ya kujitoa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa iliyotiwa saini Januari 20, 2021 ilibatilisha ombi la Marekani la Julai 6, 2020.
Rais Trump kwa amri ya Jaruari, 2025 amesema Marekani itasitisha kutoa fedha, usaidizi au rasilimali za Serikali ya Marekani kwa WHO.
Ameamuru kuwarejesha nyumbani na kuwapa kazi upya wafanyakazi wa Serikali ya Marekani au wakandarasi wanaofanya kazi katika nafasi yoyote WHO.
Amesema Serikali ya Marekani itatafuta washirika wa kimataifa wanaoaminika na wenye uwazi ili kuchukua shughuli muhimu zilizofanywa awali na WHO.
Ameishutumu WHO kwa kuruhusu ugonjwa wa Uviko -19 kushindwa kudhibitika na kupuuzia hatari ya ugonjwa huo, ambao umesababisha vifo vya maelfu ya watu duniani.
Trump ameilaumu China kwa kujaribu kuziba mlipuko huo na kuishtumu WHO kwa kushindwa kuiwajibisha China.
Amelishutumu shirika hilo kwa kuipendelea China, sehemu ya shutuma hizo zikiwa ni kutokana na upingaji wake mkali wa hatua ya Marekani kuwazuia wasafiri kutoka China kuingia nchini humo, akiita ugonjwa huo ni ”virusi vya China.”