Tanzania yaihakikishia Finland mazingira bora ya biashara, uwekezaji

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo amewahakikishia wawekezaji kutoka Finland kwamba Tanzania inaendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini.

Kombo ametoa msimamo huo leo Mei 16, 2025 jijini Dar es Salaam kwenye Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Finland, lililowakutanisha wadau mbalimbali kutoka sekta za umma na binafsi za Tanzania na Finland.

Amesisitiza dhamira ya Serikali ya Tanzania kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na Jamhuri ya Finland kwa manufaa ya pande zote.

Amesema maboresho ya mazingira ya kufanyia biashara yanalenga kurahisisha utoaji wa leseni, kupunguza urasimu na kuboresha mifumo ya forodha, ili kuongeza ufanisi wa huduma kwa wawekezaji.

Amebainisha kuwa Serikali iko tayari kushirikiana na kuhudumia wawekezaji kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Waziri Kombo ametaja teknolojia ya habari na mawasiliano, afya, dawa na teknolojia za kilimo kuwa ni miongoni mwa sekta zenye fursa kubwa za uwekezaji na ushirikiano.

Amesema Tanzania haitaki kuwa soko tu la bidhaa kutoka Finland, bali inataka kuwa mshirika wa muda mrefu na wa kuaminika katika biashara na uwekezaji.

Amewahimiza wafanyabiashara wa Kitanzania kuchangamkia fursa zilizopo katika soko la Finland na kubainisha kuwa nchi hiyo inathamini ubora, uendelevu na uwazi ambapo bidhaa za asili kutoka Tanzania zina uwezo wa kuvifikia, na hivyo kuimarisha biashara kati ya nchi hizo.

Naye Rais wa Finland, Alexander Stubb amepongeza jitihada za Tanzania za kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuelezea kuwa Finland iko tayari kushirikiana na Tanzania katika maeneo ya elimu na ufundi, nishati, afya, kilimo na mazingira kwa manufaa ya pamoja.

Rais Stubb amesisitiza kuwa Finland inaiona Tanzania kama lango muhimu kuelekea masoko ya Afrika Mashariki.

Rais huyo wa Finland ambaye ameambatana na ujumbe wa wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Finland, amehitimisha ziara yake ya siku tatu nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *