Tanzania yachomoza kriketi Afrika

WAJUMBE wa mkutano mkuu wa Afrika wa mchezo wa kriketi wameonyesha kuridhishwa na namna ya ukuzaji wake, baada ya viongozi kutoka nchi 25 kukutana Dar es Salaam.

Mkutano huo wa mafunzo umekuja wiki chache baada ya Tanzania kushinda michuano ya Divisheni ya Kwanza Afrika kwa vijana wa chini ya miaka 19 ambayo fainali zake zilichezwa jijini Lagos, Nigeria.

Kwa kushinda michuano hiyo, Tanzania pia ilifuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia kwa vijana wa umri huo.

Wakiwa Tanzania, viongozi hao walishuhudia uwekaji wa jiwe la msingi  wa uwanja mpya wa kriketi katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Wenyeviti wa vyama vya kriketi kutoka Mali, Malawi na Nigeria waliliambia Mwanaspoti kuwa wamevutiwa  na hatua ambayo Tanzania imepiga katika kujenga na kukuza kriketi ikianza vyema na mpango uitwao Kriketi Chanzo ambao ni mahsusi kwa vijana wadogo shuleni.

“Tumeona jinsi Watanzania wanavyofanya jitihada kubwa kuiendeleza kriketi.Sisi Mali tumejifunza mengi hapa na siku sio nyingi tutalipeleka somo hili nchini Mali,” alisema Kawory Berthe, mwenyekiti wa  Chama cha Kriketi Mali.

Rais wa Chama cha Kriketi cha Malawi, Vivek Ganesan alisema Malawi imejifunza kutoka Tanzania kwa muda mrefu na matokeo yake nchi yake imeanza kupiga hatua.

“Tumekuwa tukijifunza kutoka Tanzania kwa muda mrefu na  mfumo wake tumeuleta Malawi na tayari umekwishabadili sura ya kriketi nchini mwetu,” alisema Vivek.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na viongozi wa klabu za kriketi, wachezaji wa timu za taifa   na maofisa maendeleo wa kriketi.

Akizungumzia suala la ujenzi wa uwanja wa mchezo huo, Mwenyekiti wa Chama cha Kriketi Tanzania (TCA), Dk Sreekumar alisema: “Uwanja huu unategemewa kuendeleza na kukuza vipaji zaidi vya kriketi nchini  ambavyo kwa siku za baadaye zitaifanya Tanzania ipige hatua zaidi ya hii ya kushinda Kombe la Divisheni ya Kwanza kwa Bara la Afrika.”

Wakiwa nchini, viongozi wa vyama vya kriketi Afrika pia walijulishwa na chama cha kriketi nchini kuwa pamoja na ujenzi wa uwanja mpya, Tanzania pia itaboresha viwanja vingine vya kriketi nchini nzima.

Kwa sasa TCA inapiga hatua kubwa ya maendeleo katika mchezo wa kriketi ikiwa na programu maalumu ya uendelezaji vijana kuanzia katika ngazi za chini, hususan shuleni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *