
Tanzania imeanguka kwa nafasi moja katika chati ya viwango vya ubora wa soka vya Shirikisho la Mpira wa Miguu duniani (FIFA) kwa mujibu wa viwango vilivyotolewa leo, Aprili 3, 2025.
Kwa sasa Tanzania ipo katika nafasi ya 107 ikiwa na pointi 1196.04 tofauti na viwango vilivyopita vya Desemba 19, 2024 ilipokuwa nafasi ya 106 ikiwa na pointi 1199.
Anguko hilo linaonekana kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kupoteza mechi ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Morocco, Machi 25 mwaka huu kwa mabao 2-0.
Maumivu ya kuanguka katika viwango vya ubora vya FIFA hayajaikuta Tanzania pekee bali pia nchi za Uganda, Kenya, Sudan, Rwanda, Burundi, Ethiopia na Djibouti ambazo pia ni nchi wanachama wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Uganda ipo nafasi ya 89 kutoka ya 88, Kenya imeshuka kwa nafasi tatu na sasa ipo nafasi ya 111, Sudan imeshuka hadi nafasi ya 114 kutoka ya 113 na Rwanda imeshuka kwa nafasi sita, kutoka ya 124 hadi ya 130.
Burundi imetoka nafasi ya 139 hadi ya 140, Ethiopia iliyokuwa nafasi ya 146 sasa ipo nafasi ya 147 huku Djibouti ikishuka kutoka nafasi ya 191 hadi ya 192.
Nchi mwanachama wa CECAFA iliyopanda viwango ni Somalia ambayo ipo nafasi ya 201 kutoka nafasi ya 202 iliyokuwepo awali huku Sudan Kusini ikibakia katika nafasi yake ya 170.
Argentina imeendelea kutamba kileleni lakini kuna mabadiliko katika nafasi ya pili ambayo kwa chati mpya ya leo, Hispania ndio ipo hapo na nafasi ya tatu ambayo ilikuwa ikiishikilia katika viwango vilivyopita, sasa ipo Ufaransa iliyokuwa nafasi ya pili.
Nafasi ya nne imeendelea kuwepo England na Brazil imebakia katika nafasi ya tano.
Kwa Afrika, timu zilizopo katika nafasi tano za juu ni Morocco, Senegal, Misri, Algeria na Ivory Coast.