Tanzania ya tatu kuingiza nguo za mitumba Afrika, ikitumia Sh379.9 bilioni

Dar es Salaam. Tanzania imetajwa kushika nafasi ya tatu ndani ya Bara la Afrika kwa kuingiza nguo za mitumba katika mwaka 2022, ripoti ya tovuti inayojihusisha na masuala ya biashara Observatory of Economic Complexity (OEC) inaeleza.

Kwa mujibu wa tovuti hiyo, Tanzania ilitumia Sh379.921 bilioni kuingiza nguo hizo nchini huku ikitanguliwa na Ghana iliyotumia Sh418.92 bilioni na kushika nafasi ya pili, huku Kenya ikiwa kinara kwa kukamata namba moja na kutumia Sh514.6 bilioni kwenye kuagiza mitumba.

Tanzania inashika namba tatu katika orodha hii wakati ambao imeendelea kushuhudia ongezeko la mauzo ya pamba inayozalishwa katika masoko ya nje kwa miaka minne mfululizo kati ya 2020/2021.

Katika uchambuzi zaidi kupitia ripoti ya OEC nchi nyingine ili kukamilisha orodha ya nchi 10 vinara katika uingizaji wa nguo za mitumba ni Angola ambayo ilishikilia nafasi ya  nne na kutumia Sh303.93 bilioni kuagiza bidhaa hizo.

Wengine ni Nigeria iliyotumia Sh240.61 bilioni, Cameroon (Sh238.08 bilioni), Msumbiji (Sh212.75 bilioni), Benin (Sh205.15 bilioni), Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ilitumia Sh164.63 bilioni na Tunisia ambayo ikikamilisha orodha ya nchi 10 ilitumia Sh154.5 bilioni.

Mauzo ya pamba yapaa

Wakati ambao fedha nyingi zikitumika kuingiza nguo zilizotumika katika nchi mbalimbali, mauzo ya pamba katika masoko ya nje yameendelea kuongezeka.

Ripoti ya mwaka ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaonyesha kuwa mauzo ya pamba yaliongezeka kwa asilimia 52.3 kati ya mwaka 2020/2021 hadi mwaka 2023/2024.

Katika mwaka 2020/2021 mauzo ya pamba yalikuwa Sh349.5 bilioni, mwaka 2021/2022 yalikuwa Sh416.14 bilioni, mwaka 2022/2023 mauzo ya pamba yakifikia Sh510.86 bilioni na kufikisha Sh532.6 bilioni mwaka 2023/2024.

Hii ina maana gani

Akizungumzia suala hili, mchambuzi wa uchumi na biashara, Dk Balozi Morwa amesema kuzalisha pamba na kuuza nje ya nchi huku wewe ukiingiza mitumba si jambo linalopaswa kushangiliwa.

Badala yake anashauri, nguvu iongezwe zaidi katika kuvutia wawekezaji wanaotumia pamba kuzalisha nguo zinazoweza kuvaliwa na watu wa vipato tofauti, ili kuongeza wigo wa ukuaji wa uchumi na kuimarisha sarafu ya ndani.

“Kuzalisha nguo nchini na kuuza nje kutatufanya sisi kupata hela zaidi kuliko ambavyo tunauza pamba ambayo haijaongezewa thamani, tuvute wageni tuwape nafuu za kodi kwa masharti ya kutumia malighafi zinazozalishwa nchini,” amesema Dk Morwa.

Amesema hili linaweza kufanyika kwa kupitia upya misamaha ya kodi inayotolewa kwa wawekezaji kwa kuweka makundi, na si kila anayekuja wakati mwingine nchi inanufaika kidogo.

“Msamaha wa kodi utolewe kwa masharti kwamba mwekezaji atumie malighafi za ndani kuzalisha bidhaa ambayo inafaa kwa soko lililopo na lile la nje. Mwekezaji wa kuzalisha pamba tu na kuuza nje huyo asiruhusiwe,” amesema Dk Morwa.

Amesema kufanya hivi, ukuaji wa uchumi utashuhudiwa kwa mtu mmojammoja akimaanisha wakulima na wale watakaoajiriwa katika viwanda vya uzalishaji wa bidhaa, huku nchi ikinufaika kwa kupata kodi kwenye mnyororo wa bidhaa.