
Mechi ya ufunguzi ya kusaka tiketi ya kucheza michuano ya dunia ya ICC Ligi B kati ya Tanzania na Mali lilikuwa ni gumzo kubwa na majibu yake yamekuja hivi karubuni baada ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi kutangaza rasmi kujitoa katika jumuiya ya nchi zinazoongea Kifaransa.
Mali iliishangaza sana tasnia ya kriketi kwa kushiriki kikamilifu katika mchezo ambao ni mahsusi kwa nchi zinazoongea Kiingereza, Anglophone ambazo ziko katika Jumuiya ya Madola.
Mali inajiunga na Rwanda na Msumbiji, ambazo hapo awali zilikuwa katika jumuiya ya nchi zinazoongea Kifaransa na Kireno, zote mbili zilikuwepo Dar es Salaam katika michuano hiyo ya kusaka tiketi za kucheza Kombe la Dunia kwa Ligi B.
Mechi hiyo ya ufunguzi wa michuano ya kusaka tiketi ya kucheza michuano ya dunia kwa Ligi B iliyochezwa kwenye Uwanja wa Dar Gymkhana iliziweka Tanzania na Mali katika rekodi tofauti; Tanzania kupata ushindi mkubwa wa wiketi 10 na Mali kupoteza sana kwa wiketi zote 10.
Mali ambao walionekana wageni kabisa katika mchezo wa kriketi, ndiyo walioanza kubeti na kufanikiwa kutengeneza mikimbio 18 tu baada ya wote 10 kutolewa wakiwa wametumia mizunguko 12 kati ya 20 iliyowekwa.
Tanzania ilijibu vyema alama hizi dhaifu kwa kutengeneza mikimbio 19 bila ya kupoteza wiketi ikiwa imetumia mizunguko 0.5 kati ya 20 na hivyo kuondoka ma ushindi wa wiketi zote 10.
Sanze Kamate na Yacouba Konate ndiyo waliocheza vizuri kwa Mali baada kila mmoja wao kutengeneza mikimbio 3 tu.
“Mali ndiyo kwanza wameanza kucheza kriketi, nafikiri miaka ya baadaye watakuwa wazuri baada ya mchezo kukomaa,” alisema msemaji wa chama cha kriketi nchini (TCA) Ateef Salim.
Michuano ya kusaka tiketi ya Kombe la Dunia kwa vijana wa chini ya miaka 19 iliwaleta Rwanda na Msumbiji jijini Dar es Salaam.
Tanzania ambayo ilishinda mechi zake zote na kukata tiketi, ilianza kwa kuifunga Nigeria kabla ya kuwatoa Ghana na Msumbiji katika michezo mingine ya hatua ya makundi.
Tanzania ilitinga fainali baada ya kuitoa Rwanda katika mchezo wa nusu fainali na mwisho iliizamisha Siera Leone kwa mikimbio 38 katika mechi ya fainali.
Kwa kuangalia mifano ya Mali, Rwanda na Msumbiji, kriketi imeonekana kama ni kitambusho kikubwa cha nchi zinaongea Kiingereza. Ingawa Mali haijatangaza rasmi kuwa ni mwanachama wa Commonwealth baada ya kijitoa umoja wa nchi zinazongea Kifaransa (Francophone) inaweza kujiunga na jumuiya ya nchi zinazoongea Kiingereza endapo hatua za makusudi zitachukuliwa.
Msumbiji tayari ni mwanachama wa Jumuiya ya Madola na tayari imekwisha shiriki katika michezo hiyo mara kadhaa. Michezo mingine inayobeba bendera ya nchi za Jumuiya ya Madola ni mpira wa pete, mpira wa vinyoya (badminton), hockey (mpira wa magongo), mbio za magari (Safari Rally) ambazo ziliasisiwa mwaka 1953 kama kumbukumbuku ya kutawazwa kwa Malkia Elizabeth wa Uingereza na kupitia katika nchi za Kenya, Tanzania na Uganda.