Tanzania, Sweden kupambana na athari za viuatilifu nchini

Arusha. Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania  (TPHPA), imeingia makubaliano ya miaka miwili na Taasisi  ya Udhibiti wa Kemikali ya Sweden (Kemi) kukabiliana na athari za viuatilifu kwa afya za binadamu, wanyama na mazingira kwa jumla.

Akizungumza leo Jumatatu, Aprili 14, 2025 jijini Arusha baada ya kusaini hati ya makubaliano hayo (MoU), Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru amesema ushirikiano huo pia utajikita katika ufanyaji utafiti wa viatilifu hai.

Amesema lengo ni kudhibiti visumbufu mbalimbali vya mazao ili kukabiliana na usugu wa baadhi ya sumu hizo.

“Ushirikiano huo unaenda sambamba kwenye maeneo matatu ambayo ni udhibiti wa viuatilifu ili kulinda afya ya walaji na mazingira, kutengeneza miongozo kwa ajili ya udhibiti wa viuatilifu na kuangalia matumizi ya mifumo ya kimataifa katika kutambua kemikali na kuweka nembo,” amesema.

Profesa Ndunguru amesema ushirikiano huo ni mwendelezo wa Sweden kuisaidia Tanzania katika ustawi wake katika sekta ya kilimo.

Amesema awali, wataalamu kutoka TPHPA waliokuwa wakienda kupata mafunzo Sweden ya kudhibiti matumizi ya viuatilifu, nao walifika nchini kufanya utafiti.

Hivyo, Profesa Ndunguru amesema makubaliano waliyosaini, yataendelea kuleta tija kwa nchi hasa katika usalama wa afya za walaji, wanyama na mazingira, kwa kuwa na matumizi sahihi na salama ya viuatilifu kwa ustawi mzuri wa sekta ya kilimo.

Msimamizi wa mradi kutoka Kemi, Raphael Mwezi amesema ushirikiano wa Sweden na Tanzania katika kudhibiti sumu ya viuatilifu, ulianza tangu mwaka 2018.

Mwezi amesema tayari Tanzania imefanikiwa kupata fursa ya kubadilishana uzoefu na wataalamu kutoka Sweden sambamba na kupeana mafunzo na mbinu za usimamizi wa viuatilifu.

“Ushirikiano wa awali, uliisha mwaka 2024, wenzetu waliona kuna umuhimu tena wa kuingia kwenye makubaliano haya mapya ili kusaidia kudhibiti athari za viuatilifu hasa vyenye usugu, lakini vyenye madhara kwa afya za binadamu, wanyama na mazingira kwa ujumla,” amesema.

“Katika makubaliano ya sasa tunakwenda kupeana mafunzo ya utendaji kazi, usimamizi wa mikataba ya kimataifa yanayohusu kemikali na kujengeana uwezo wa usimamizi wa viatilifu ikiwamo mfumo mzima kuanzia usajili hadi kuweka vibandiko,”amesema Mwezi.

 Meneja wa kitengo cha usimamizi wa teknolojia ya unyunyiziaji  wa viuatilifu TPHPA, Dk Magreth Francis amesema ni furaha kushirikiana  na Kemi katika majukumu yao yatakayoisaidia nchi kukabiliana na athari za kemikali katika ardhi inayohatarisha pia usalama wa bioanuai ya udongo.

“Hii pia itapanua soko la mazao ya Tanzania kwenda nchi nyingi za Ulaya kwa sababu yatakuwa hayana madhara ya kemikali ambayo imekuwa ikiziondolea sifa bidhaa nyingi katika soko huru la Afrika,” amesema.

Ernest Shayo mmoja wa wakulima nchini, amesema changamoto kubwa katika shughuli zao za kilimo ni usugu wa viuatilifu ambavyo vimekuwa vikiwapa hasara ya mavuno kwa asilimi 30 mpaka 60.

“Tunaomba Serikali pia iongeze ujuzi kwa wataalamu wetu wa ugani wanaotutembelea, wengi wanakuja shambani kuona tatizo, lakini wanashindwa kung’amua suluhu hadi madhara yanapoanza kuwa makubwa, ndio wanaleta wataalamu wa ziada wakati hasara imeshatokea,” amesema Shayo.

Helena Paul ameiomba Serikali kufanya utafiti wa kuleta viuatilifu mbadala wa vile vilivyokaa muda mrefu sokoni na kugeuka sumu shambani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *