
Baada ya kusaka ushindi katika mechi nane mfululizo bila mafanikio, hatimaye Tanzania Prisons imeikandamiza Kagera Sugar na kumtibulia rekodi Kocha Juma Kaseja.
Kabla ya ushindi huo wa bao 1-0, Tanzania Prisons ilicheza mechi nane mfululizo ikiwamo moja ya Kombe la Shirikisho (FA) ikipoteza saba na sare moja na leo Aprili 6, 2025 imeibuka na alama tatu na kufikisha 21.
Matokeo hayo yanaifanya timu hiyo kuweka rekodi ya kuifunga Kagera Sugar ambayo tangu ipande Ligi Kuu 2004, haijawahi kupoteza mechi kwenye Uwanja wa Sokoine.
Kama haitoshi, Maafande hao wamekuwa wa kwanza kumsimamisha Kaseja aliyekabidhiwa Kagera Sugar akiiongoza mechi nne na kushinda zote ikiwamo ya Kombe la Shirikisho (FA) tangu achukue nafasi ya Melis Medo.
Katika mechi hiyo ambayo imeanza saa 8 mchana, timu zote zilionekana kuwa na kasi kubwa katika kutafuta ushindi zikishambuliana mwanzo mwisho.
Tanzania Prisons ilisubiri hadi dakika ya 61 kupata bao kupitia kwa Haruna Chanongo aliyetumia vyema pasi fupi ya Beno Ngassa na kuukwamisha mpira wavuni.
Kagera Sugar waliendelea kulisaka lango la Tanzania Prisons lakini kipa Mussa Mbisa alikuwa imara langoni na kufanya dakika 90 kumalizika kwa wenyeji kubaki na alama tatu ikiendelea kusalia nafasi ya 15.
Kocha Kaseja amesema kupoteza mchezo huo ni kutokana na ugumu wa wapinzani kwani kila timu ilihitaji ushindi na kwamba anawapongeza wachezaji jinsi wanavyopambana kuinusuru timu na janga la kushuka daraja.
“Prisons walihitaji ushindi kwakuwa nafasi tuliyopo na waliyopo wao ilikuwa lazima upinzani uwepo, kiujumla sijaweka chochote zaidi ya vijana wenyewe kuamua kupambana, tunaenda kujipanga na mechi zinazofuata,” amesema kocha huyo.
Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Aman Josiah amesema wamekuwa katika kipindi kigumu cha matokeo licha ya kwamba kiwango kimekuwa si cha chini akiwaomba wadau na mashabiki kuungana kipindi hiki kuinusuru timu.
“Timu ilikuwa inacheza vizuri, hatukukosa matokeo kwa sababu ya kiwango, kwa ujumla niwapongeze wachezaji na sasa kila mmoja kwa nafasi yake tushirikiane timu ibaki Ligi Kuu.
“Kwa sasa hatuangalii cha rekodi wala historia kwakuwa benchi ni jipya na wachezaji wengine hawakuwepo misimu ya nyuma, hivyo kila mchezo ni fainali,” amesema Josiah.