Tanzania Prisons, KMC zafufua matumaini zikipata ushindi

Dar es Salaam. Matumaini ya Tanzania Prisons na KMC kusalia Ligi Kuu Tanzania Bara yamezidi kuwa hai baada ya timu hizo kuibuka na ushindi katika mechi zilizocheza nyumbani dhidi ya JKT Tanzania na Dodoma Jiji FC.

Tanzania Prisons licha ya kutanguliwa kwa mabao mawili na JKT Tanzania, imepambana vilivyo nyumbani kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya na kuibuka na ushindi wa mabao 3-2.

Shujaa wa Tanzania Prisons katika mechi ya leo alikuwa ni Oscar Mwajanga aliyefunga mawili huku lingine likipachikwa na Jeremiah Juma wakati mabao mawili ya JKT Tanzania yamefungwa na Mohammed Bakari na lingine lilikuwa la kujifunga la Jumanne Elfadhil.

Katika mchezo huo, Adam Adam alikosa mkwaju wa penalti ambao uliokolewa na kipa wa JKT Tanzania, Yakoub Suleiman.

Kwa ushindi huo, Tanzania Prisons imefikisha pointi 27 lakini bado ipo nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi wakati JKT Tanzania imeshuka kwa nafasi moja hadi ya nane ikiwa na pointi 32.

Kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge Dar es Salaam, mabao ya Abdallah Said na Rashid Chambo yametosha kuipa ushindi wa mabao 2-1 KMC dhidi ya Dodoma Jiji ulioifanya ifikishe pointi 33 na kupanda hadi nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi.

Bao pekee la Dodoma Jiji ambayo imebaki katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 34, limepachikwa na Iddi Kipagwile.

Baada ya mechi ya leo, Tanzania Prisons imebakisha michezo mitatu ambayo miwili ni dhidi ya Coastal Union na Yanga na mmoja ugenini dhidi ya Singida Black Stars.

Kwa upande wa JKT Tanzania, imebakisha mechi mbili nyumbani dhidi ya Simba na Fountain Gate na ina mechi mbili ugenini dhidi ya Pamba Jiji FC na Mashujaa FC.

KMC imebakisha mechi nne ambazo ni moja nyumbani dhidi ya Simba na tatu ugenini dhidi ya Tabora United, Mashujaa FC na Pamba Jiji FC.

Dodoma Jiji imebakiza mechi tatu ambazo ni mbili ugenini dhidi ya Azam FC na Yanga na moja nyumbani dhidi ya Singida Black Stars.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *