
Dar es Salaam. Tanzania na Namibia zimekubaliana kukuza ushirikiano wa kibiashara baina yao ambao bado uko chini licha ya kwamba umeongezeka thamani katika miaka ya karibuni.
Mbali na ushirikiano katika biashara, uhusiano huo pia utajikita katika sekta muhimu ikiwemo uchumi wa buluu ambao Namibia inafanya vizuri pamoja na sekta za gesi na mafuta.
Hayo yamebainishawa usiku wa jana Jumanne Mei 20, 2025 katika mkutano na vyombo vya habari uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam kati ya Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania pamoja na Rais wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah.
Rais Nandi-Ndaitwah amefanya ziara ya kiserikali ya siku mbili nchini Tanzania kuanzia jana Mei 20 hadi leo Jumatano 21, 2025 kwa mwaliko wa Rais Samia.
Hii ni ziara ya kwanza ya Rais Nandi-Ndaitwah nchini Tanzania tangu aapishwe kuwa Rais wa Namibia Machi 21, 2025 na ziara hiyo inalenga kukuza ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na kijamii, ikiwemo katika nyanja za biashara, uwekezaji na elimu.
Siku anaapishwa, Rais Samia alikuwa mgeni maalumu kwenye shughuli hiyo nchini Namibia.
Tanzania na Namibia zimejenga uhusiano wa muda mrefu wa kidugu na kidiplomasia, hivyo ziara hii itafungua fursa mpya za ushirikiano zitakazowawezesha wananchi wa nchi zote mbili kunufaika kiuchumi.
Rais Nandi-Ndaitwah alipokelewa Ikulu ya Dar es Salaam na mwenyeji wake, Rais Samia, ambapo walikuwa na mazungumzo ya wawili na kisha kuongoza mazungumzo rasmi baina ya nchi hizo mbili na baadaye kuzungumza na waandishi wa habari.
Akizungumza na vyombo vya habari baada ya mazungumzo yao, Rais Samia amesema wamekubaliana kuenzi na kuendeleza uhusiano ulioanzishwa na waasisi wa mataifa yao, Mwalimu Julius Nyerere na Sam Nujoma.
Amesema ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Namibia uko chini ingawa umekuwa ukiongezeka kutoka thamani ya Sh17 bilioni mwaka 2019 hadi kufikia Sh20 bilioni mwaka 2023.
“Katika mazungumzo yetu, tumeangazia fursa tunazoweza kuzitumia kukuza uhusiano wetu wa kibiashara. Nimewaalika wafanyabiaahara wa Namibia kushiriki katika maonyesho ya Sabasaba mwaka huu,” amesema Rais Samia.
Kiongozi huyo amebainisha kwamba wamependekeza kuangalia eneo la uongezaji thamani hasa wa mazao ya mifugo na utalii kwa manufaa ya nchi zao.
Kwa upande wa gesi na mafuta, Rais Samia amesema mataifa yote mawili yana rasilimali hizi na Namibia imeanza kunufaika na mafuta, hivyo wamezielekeza taasisi zinazosimamia sekta hiyo kushirikiana na kubadilishana uzoefu.
“Eneo lingine tumejadiliana kuhusu uchumi wa buluu, tumekubaliana tuutumie kutatua tatizo la ajira katika nchi zetu. Namibia inafanya vizuri katika sekta hii, hivyo Tanzania tungependa kupata uzoefu katika matumizi ya rasilimali za bahari,” amesema.
Amebainisha jambo jingine walilokubaliana ni kukuza lugha ya Kiswahili na kuitumia kwa maendeleo ya kiuchumi. Katika kutekeleza hilo, wamekubaliana lugha hiyo kuanza kufundishwa katika chuo kikuu kimoja nchini Namibia.
Kwa upande wake, Rais Nandi-Ndaitwah amemshukuru Rais Samia kwa kukubali kwenda kuhudhuria siku ya kumbukizi ya uhuru wa Namibia na kuwa mgeni rasmi na mzungumzaji katika hafla ya kuapishwa kwake kama Rais wa nchi hiyo.
Amesema yuko hapa nchini kujifunza na kubadilishana uzoefu katika kuwatumikia wananchi wao. Ameongeza anatambua mchango mkubwa wa Tanzania katika kupigania ukombozi wa Afrika.
Kuhusu waliyokubaliana kwenye mazungumzo yao, amesema uchumi wa buluu ni sekta muhimu ambayo ikitumika vizuri inaweza kubadilisha maisha ya wananchi, hivyo watashirikiana katika eneo hilo ambalo lina nafasi kubwa katika uchumi wa nchi yake.
Pia, amesisitiza umuhimu wa kuongeza thamani kwenye mazao na katika mnyororo wa thamani ili mataifa yao yapige hatua kubwa kiuchumi na kushindana katika soko huria.
“Tumekuwa na mazungumzo kuhusu maeneo ya ushirikiano, lakini yote kwa ujumla yanalenga kutengeneza ajira hasa kwa vijana ambao wana matarajio makubwa kutoka kwetu,” amesema Rais Nandi-Ndaitwah.
Kadhalika, amesema wamekubaliana kuchochea sekta binafsi kushiriki katika kukuza uchumi na kwamba atakwenda kuwahamasisha wafanyabiashara wa Namibia kushiriki katika maonyesho ya Sabasaba.
“Hivi karibuni nitawatuma mawaziri wangu wa biashara na viwanda kuja kujifunza namna Tanzania ilivyopiga hatua kwenye maeneo hayo,” amesema kiongozi huyo mwanamke wa kwanza katika nchi ya Namibia, akiwa ni Rais wa tano.
Katika siku ya pili na ya mwisho ya ziara yake hapa nchini, leo Jumatano, Rais Nandi-Ndaitwah pamoja na mambo mengine atatoa mhadhara Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.