
Dar es Salaam. Washiriki zaidi ya 1,000 kutoka nchi mbalimbali ikiwemo za Afrika ya Mashariki, wanatarajia kujifungia kwa siku tatu nchini kujadili mchango wa rasilimali za mafuta na gesi asilia katika maendeleo endelevu ya Afrika Mashariki na fursa za uwekezaji zilizopo.
Washiriki hao watatumia Machi 5 hadi 7 mwaka huu kupitia Maonyesho ya 11 ya Petroli ya Afrika Mashariki (11TH East African Petroleum Conference and Exhibition – EAPCE25).
Mkutano huu unatarajiwa kuzinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan huku ukitanguliwa na mafunzo yanayotarajiwa kufanyika Machi 4, jijini hapa.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Ijumaa, Februari 7, 2025, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba amesema mkutano huo wa EAPCE25 utawaleta pamoja watunga sera, viongozi wa serikali kutoka nchi mbalimbali ikiwemo nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wawekezaji wa kimataifa na wa ndani.
Mramba ameeleza kuwa mada mbalimbali kutoka kwa wataalamu na wabobezi katika sekta ya mafuta na gesi zitatolewa zikiwemo utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi katika nchi za Afrika Mashariki.
“Pamoja na hayo kutakuwa na fursa za uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa mafuta na gesi, dhana ya kuelekea nishati safi, masuala ya mazingira, miundo ya kisera, kisheria na kiudhibiti katika mafuta na gesi na masuala mengine muhimu kwa sekta hiyo,” amesema.
Mkutano huu unatajwa kuwa fursa muhimu kwa wafanyabiashara kwani utahusisha maonyesho ya bidhaa na huduma kutoka kampuni mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa mafuta na gesi asilia.
“Mkutano wa EAPCE25 unafanyika katika wakati muhimu hasa baada ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika kujadili masuala ya nishati,” amesema.
Katika mkutano wa nishati uliofanyika Januari 27 na 28 jijini hapa ukibeba ajenda 300 nchi za Afrika zilikubaliana kuweka mpango mahususi wa Taifa wa nishati kwa kipindi cha miaka mitano 2025-2030 ambapo kwa Tanzania mpango uliopo ni kuunganisha watumiaji wa umeme kufikia asilimia 75.
Pia mkakati mwingine uliowekwa na Tanzania katika mkutano huo ni kuongeza kiwango cha upatikanaji umeme kufikia asilimia 100 na kuwezesha matumizi ya nishati safi ya kupikia kufikia asilimia 80 ifikapo mwaka 2030.
Mramba ameongeza kuwa ili kufikia malengo yaliyowekwa kupitia mkutano wa Nishati Afrika, nchi inahitaji kutumia rasilimali za asili ikiwemo za mafuta na gesi ili kuchangia katika upatikanaji wa nishati ya uhakika ikiwemo nishati safi ya kupikia.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kikanda ya maandalizi ya EAPCE25 ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi, Dk James Mataragio amesema mkutano huu utahusisha ziara za kitaaluma katika maeneo ya kijiolojia katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuwapa washiriki mtazamo wa vitendo kuhusu sekta.
Amesema ziara hizo zitatoa fursa ya kuona miradi inayoendelea na mipango ya baadaye.
“Hili litawezesha wawekezaji na wadau kubaini fursa za biashara na ushirikiano katika sekta ya nishati katika ukanda wa Afrika Mashariki,” amesema Dk Mataragio.
Kuhusu utaratibu wa kushiriki katika mkutano wa EAPCE25, Mwenyekiti wa kamati ya Kitaifa ya maandalizi, Joyce Kisamo amezitaka kampuni na wadau mbalimbali wa sekta ya mafuta na gesi kujiandikisha kushiriki katika mkutano huu na pia kutumia nafasi hii kutangaza bidhaa na huduma zao kupitia maonesho.
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inajumuisha nchi wanachama wanane Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Somalia, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zenye jumla ya idadi ya watu zaidi ya milioni 300.