Tanzania: Majimbo mapya nane ya uchaguzi yauundwa na tume ya uchaguzi

Tume huru ya uchaguzi nchini Tanzania, Jumatatu ya wiki hii ilitangaza uundwaji wa majimbo mapya nane ya uchaguzi, ambapo sasa yanafanya nchi hiyo kuwa na jumla ya majimbo 272 kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Imechapishwa: Imehaririwa:

Dakika 1

Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa tume hiyo jaji mstaafu Jacobs Mwambegele, hatua hii imekuja kufuatia maoni ya wadau yaliyotolewa kuanzia Februari 26 hadi machi 2 mwaka huu.

Katika taarifa yake, jaji Mwambegele amesema tume ilizingatia vigezo kadhaa kuamua ikiwemo idadi ya watu wanaozidi laki 6 katika maeneo ya miji na laki 4 katika maeneo ya vijijini.

Hata hivyo tangazo hili tayari limeibua mjadala miongoni mwa raia, baadhi wakihoji haja na ulazima wa kuongeza majimbo huku wengine wakiunga mkono.

Kwa muda sasa mashirika kadhaa ya kiraia na vyama vya upinzani nchini Tanzania, yamekuwa  yakipinga kuongezwa kwa idadi ya wabunge, baadhi wakipendekeza hata idadi iliyopo sasa kupunguzwa.

Kwa sasa bunge la Tanzania lina jumla ya wabunge 397 wakuchaguliwa na viti maalum, na nyongeza ya majimbo 8 ina maanisha kutakuwa na wabunge 405.

Kati ya majimbo 272, 222 yako Tanzania bara huku 50 yakiwa Zanzibar.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *